Trump: Mkataba na Taliban umekaribia
14 Februari 2020Waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper ametangaza kufikiwa makubaliano hayo baada ya mkutano wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Brussels siku moja tangu rais Ashraf ghani wa Afganistan aliarifu kuwa mazungumzo kati ya Marekani na Taliban yamepiga hatua muhimu.
Esper hakusema ni lini hasa makubaliano hayo madogo yataanza kutekelezwa lakini afisa mmoja wa kundi la Taliban ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kundi litaangaza kupunguza machafuko yanayotokana na shughuli zake za kijeshi leo Ijumaa.
Zaidi kuhusu makubaliano hayo waziri Esper amesema "ni mtizamo wetu kwamba siku saba zitatosha hivi sasa lakini kwa ujumla mwelekeo wetu kwenye mchakato huu unaandamana na masharti. kwa hiyo utakuwa ni mchakato unaoendelea kufanyiwa tathmini kadri tunavyosonga mbele, kama tutasonga mbele"
Esper amesema Marekani bado inaamini njia pekee ya kumaliza ghasia nchini Afghanistan ni kupitia maridhiano ya kisiasa na kuahidi kutoa taarifa pana kuhusu hilo katika siku chache zinazokuja.
Trump asifu hatua iliyopigwa
Tangazo la waziri Esper linatolewa baada ya rais Donald Trump wa Marekani kusema jana kuwa nchi yake imekaribia kufikia mkataba wa amani na kundi la wanamgambo la Taliban la nchini Afghanistan.
Trump amekiambia kituo kimoja cha radio nchini Marekani kwamba kuna uwezekano wa kupatikana mkataba na Taliban lakini suala hilo litafahamika katika kipindi cha wiki mbili zinakuja.
Kiongozi huyo ameitaja hatua iliyopigwa kuelekea makubaliano kuwa nafasi muhimu kwa pande hizo mbili zaidi ya miaka 18 tangu marekani ilipoivamia Afghanistan na kuipundua serikali ya Taliban baada ya kutokea mashambulizi pacha ya kigaidi ya Septemba 11.
Pompeo kujadiliana na Ghani mjni Munich
Katika hatua nyingine waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amesema akiwa njiani kuelekea kwenye mkutano wa usalama wa mjini Munich kuwa mazungumzo kati ya nchi yake na Taliban yamepiga hatua muhimu siku chache zilizopita.
Wakati wa mkutano wa Munich, Pompeo anatarajiwa kukutana na rais Ashraf Ghani wa Afghanistan kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana katika mazungumzo hayo ya mjini Doha, Qatar.
Washington na Taliban wamekuwa kwenye mkwamo katika mazungmzo yaliyochukuwa zaidi ya mwaka mmoja yanayofanyika mjini Doha nchini Qatar.
Iwapo yatafanikiwa, makubaliano hayo yatayowezesha Marekani kuviondoa vikosi vyake nchini Afghanistan na kundi la Taliban litatoa hakikisho la kuwepo usalama na kuanzisha mazungumzo na serikali ya mjini Kabul.