1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Clinton watafuta kura katika majimbo matano

Caro Robi26 Aprili 2016

Wamarekani katika majimbo matano ya kaskazini mashariki watapiga kura hii leo katika uchaguzi wa mchujo wa kuteua wagombea urais wa vyama vya Republican na Democratic.

Picha: Reuters/D. Becker/N. Wiechec

Mgombea Urais wa chama cha Democrats Hillary Clinton ataazimia katika chaguzi hizo za leo kupanua pengo kati yake na Bernie Sanders huku mgombea urais kwa upande wa Republican Donald Trump akiwa na uhakika wa kuendelea kuongoza katika kinyang'anyiro cha kupata tiketi ya chama chake licha ya wapinzani wake kuungana dhidi yake.

Chaguzi hizo za mchujo zinafanyika katika majimbo ya Connecticut, Delaware, Maryland, Pennsylvania na Rhode Island. Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Bi Clinton anatumai kuibuka na ushindi katika majimbo hayo na hivyo kuendeleza ndoto yake yake ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini Marekani.

Clinton ana imani atashinda

Akihutubu katika jukwaa la manispaa ya Philadelphia jana usiku, Clinton amesema bado hawajapata uteuzi na hivyo watatia bidii sana kuwashawishi wapiga kura hadi vituo vitakapofungwa.

Mgombea Urais wa Democrats Bernie SandersPicha: Reuters/L. Jackson

Trump pia alikuwa akifanya kampeni kabambe katika majimbo hayo matano muhimu kujaribu kufikisha idadi ya wajumbe 1,237 wanaohitajika kumuwezesha kupata tiketi ya kupeperusha bendera ya chama cha Republican katika uchaguzi wa Rais unaotarajiwa mwezi Novemba mwaka huu.

Wapinzani wake Ted Cruz na John Kasich wameungana kujaribu kutatiza ndoto ya Trump ya kugombea urais.

Kulingana na mapatano kati ya wagombea hao wawili, Kasich hatafanya kampeni katika jimbo la Indiana ambalo linafanya uchaguzi wa mchujo tarahe 3 mwezi ujao na kwa upande wake Cruz hatatafuta kura katika majimbo la New Mexico na Oregon ili kuzigawanya kura ambazo angepata Trump.

Trump amewakosoa wapinzani wake kwa kula njama ya kumbwaga akisema mapatano yao yanaonyesha ni kwa kiasi gani wako dhaifu na wanatapatapa.

Cruz na Kasich waungana kumbwaga Trump

Kulingana na taifiti za kura ya maoni ziliofanywa na shirika la habari la CBS, Trump anaongoza kwa asilimia 40 kwa umaarufu miongoni mwa wapiga kura Indiana, huku Cruz akiungwa mkono kwa asilimia 35 na Kasich asilimia 20.

Wagombea urais wa Republican Trump, Cruz na KasichPicha: picture-alliance/AP Photo/P.Sancya

Cruz na Kasich wamekiri kuwa matumaini yao ya kuibuka washindi ni kuungana katika kumzuia Trump kupata wajumbe 1, 237 kabla ya mkutano mkuu wa chama.

Cruz hata ameanza kutafuta mgombea mwenza. Mwenyekiti wa kampeini zake Chad Sweet amesema Cruz ameanza kuwatathimini wagombea kadhaa watakaochukua wadhifa wa makamu wa Rais akiwemo mfanyabiashara Carly Fiorina.

Trump anapigiwa upatu kushinda katika majimbo yote matano yanayoshiriki katika chaguzi za mchujo leo naye Sanders ambaye kampeni zake mashinani zimeshika kasi, anabashiriwa atajitahidi vilivyo kumtoa kijasho Clinton hasa katika jimbo la Connecticut.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW