1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Macro wakutana katika Ikulu ya Marekani

24 Aprili 2018

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe Brigitte wapo katika Ikulu ya Marekani mjini Washington katika ziara rasmi ya siku tatu. Pamoja na mengine Trump na Macro watajadili mkataba wa nyuklia wa Iran.

USA Washington - Donald Trump trifft Emmanuel Macron
Picha: Reuters/J. Roberts

Rais Emmanuel Macron na mkewe walipokewa katika ikulu ya Marekani na mwenyeji wao Rais Donald Trump pamoja na mke wake, Melania Trump, ambao ni wenyeji wa ziara ya kwanza rasmi tangu Trump aiingie madarakani miezi 15 iliyopita. Marais hao wawili Trump na Macron walisalimiana kwa kupeana mikono na kubusiana mashavuni kabla ya kusimama wima kwa wimbo wa mataifa yao.

Katika hotuba yake katika Ikulu ya White House, Trump amesema urafiki mzuri aliouanzisha na Ufaransa ni ushuhuda kuwa nchi hizo mbili zina muungano wa kweli. Trump pia amemshukuru Macron kwa ushirikiano wake wa haraka wa kuyajibu mashambulizi ya kemikali za sumu nchini Syria.

Rasi wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha: Reuters/J. Bourg

Rais huyo wa Marekanina mwenzake wa Ufaransa wanakutana kwa majadiliano  juu ya mambo tofauti yakiwemo mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran na mgogoro wa Syria.

Aidha masuala ya kibiashara pia yatajadiliwa. Umoja wa Ulaya unataka kuondolewa katika mpango wa Trump wa kutozwa ushuru wa asilimia 25 kwa uingizwaji wa  bidhaa za chuma na bati.

Jengine lililo katika ajenda ni lile la Rais Trump kutaka kuondoa jeshi la Marekani nchini Syria haraka iwezekanavyo.

Macron ataka kumshawishi rais Trump kuukumbatia mkataba wa silaha za nyuklia wa Iran

Lakini kikubwa kitakachojadiliwa katika ziara hii ya Macron nchini Marekani ni uwezekano wa kumshawishi Trump kuuhifadhi mkataba wa nyuklia wa Iran uliotiwa saini mwaka 2015 ambao Trump ameonya kuufutilia mbali iwapo hakutakuwepo na marekebisho ifikapo tarehe 12 mwezi Ujao.

Macron ambaye ziara yake itafuatiwa na ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Marekani siku ya Ijumaa kuzungumzia suala lilo hilo, anauona mkataba wa nyuklia wa Iran kuwa chaguo zuri lililopo kwa sasa ili kuizuwiya Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Rasi wa Marekani Donald Trump na mkewe Melania Trump wakiwa pamoja na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mke wake Brigitte MacronPicha: Reuters/J. Ernst

Huku hayo yakiarifiwa onyo kali limetolewa na Rais Hassan Rouhani wa Iran dhidi ya  makubaliano ya nyuklia. "Mtu yeyote atakayekiuka makubaliano yaliyopo atapambana na majibu makali," alisema Rouhani huku akisisitiza kuwa  nchi yake iko tayari kupambana na hali yoyote ile.

Kando na hilo, Rais Emmanuel Macron amemtaka Trump kuendelea kuyaweka majeshi yake nchini Syria ili kupambana na wanamgambo wa dola la kiislamu. Amemwambia Trump kwamba kwa pamoja Ufaransa na Marekani watashinda vita dhidi ya Ugaidi.

Baada ya vikao vya leo, Trump na Macron watajumuika pamoja  na wajumbe wengine 150 kwa karamu ya chakula cha jioni. Kilele cha ziara ya Macro ni hapo kesho wakati atakapohutubia kikao cha pamoja cha mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani Congress.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW