1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia kusitisha uhusiano na China kisa ni corona

15 Mei 2020

Rais Donald Trump ameashiria kudhoofika zaidi kwa uhusiano kati ya  Marekani na China kuhusiana na mripuko wa virusi vya corona na kudai kwamba hawezi kuzungumza na rais Xi Jinping wa China kwa hivi sasa.

US Präsident Trump
Picha: picture-alliance/CNP/A. Harrer

Trump amependekeza kwamba anaweza hata kukatisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili. Wakati huo vifo vilivyotokana na maradhi hayo ulimwenguni kote vimepindukia 300,000. Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Fox Business, Trump alisema kwamba anasikitishwa sana namna China ilivyoshindwa kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 na kwamba janga hilo limeweka wingu katika makubaliano ya biashara ya mwezi Januari na Beijing, ambayo hapo awali aliyasifu kuwa ni mafanikio makubwa. "Hawakupaswa kuacha hili litokee", alisema Trump na kuongeza kwamba.

"Jambo baya lilitokea na unaweza kulitazama kama chanzo ni China, lilitokea wakati fulani na lingeweza kuzuiliwa. Tuliwaomba kama tunaweza kwenda na wakasema hapana, hawakutaka msaada wetu. Hivyo nilifikiria nikasema sawa, kwasababu wanajua wanachokifanya. Kwahiyo ilikuwa ama ni ujinga au kutokuwa na uwezo, au ilikuwa makusudi, moja kati ya hizo", alisema Trump.

Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China Zhao Lijian amewaeleza waandishi wa habari mjini Beijing kwamba kuendeleza mahusiano ya pande mbili ni katika maslahi ya watu wote na kwamba yatakuwa na manufaa kwa usalama na utulivu wa dunia. "Zote China na Marekani sasa zinapaswa kushirikiana kukabiliana na kirusi kwa pamoja, kuwatibu wagonjwa na kurejea katika shughuli za kiuchumi, lakini hili linahitaji Marekani iwe na dhamira ya kufanya kazi na sisi", alimalizia Zhao. Hadi sasa Marekani  imerekodi vifo takribani 86,000 vinavyohusiana na COVID-19, ikiwa ni idadi ya juu kuliko taifa lolote.

Donald Trump na Xi Jinping mwaka 2017Picha: Getty Images/AFP/N. Asfouri

Shughuli katika mataifa mengi ya Ulaya zinaanza kurejea kawaida. Austria na Ujerumani zinatarajiwa kufungua mipaka yake hii leo, wakati Latvia, Lithuania na Estonia nazo zikijaribu kuweka mpango wake wenyewe wa kuruhusu watu kusafiri kwa uhuru ndani ya nchi hizo tatu. Lakini huko Amerika ya Kusini, hali bado ni tete. Maelfu ya makaburi yanaendelea kuchimbwa katika mji mkuu wa Chile, Santiago wakati maambukizi yakizidi. Mexico imeripoti ongezeko kubwa la maambukizi ndani ya siku moja na kufikia 2,409.

Kisa cha kwanza kimethibitishwa katika kambi za wakimbizi zilizofurika za warohingya kusini mwa Bangladesh ambako zaidi ya wakimbizi milioni moja wanapewa hifadhi. Wakati huo shirika la afya ulimwenguni WHO limeitaka Madagascar kuifanyia majaribio ya kisayansi tiba yake ya mitishamba ambayo rais wake Andry Rajoelina anadai kwamba inatibu ugonjwa wa COVID-19.

Mkuu wa shirika hilo barani Afrika Matshidiso Moeti alisema hapo jana kwamba "wamejitolea kuunga mkono utafiti wa tiba hiyo". Tayari WHO imekutana na rais na waziri wa afya wa Madagascar kujadili ni mazingira gani utafiti huo unaweza kuendeshwa ili kubaini ufanisi wake. "Hatuipingi bidhaa hiyo lakini tungependa ijaribiwe. Ili tutakapoifanya iweze kupatikana kimataifa tuwe tayari na ushahidi", alisema mkurugenzi huyo. Tiba hiyo ya asili iliyopewa jina la Covid Organics inatengenezwa na mmea aina ya artemisia.

Vyanzo: Reuters/AP/DPA