1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump, Pence waahidi kushirikiana kumaliza muhula wao

12 Januari 2021

Rais wa Marekani Donald Trump na makamu wake Mike Pence wamekutana Jumatatu kwa mara ya kwanza tangu wafuasi wa Trump walipovamia bunge wiki iliyopita, na kuahidi kuendelea kufanya kazi wote ili wakamilishe muhula wao.

US Wahl 2020 Donald Pence Trump
Picha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

Mkutano huo katika ofisi ya rais ulioelezwa na afisa wa juu kuwa mazungumzo mazuri, ulikuja kuelekea kipindi kizito cha masaa 48 wakati ambapo Pence anakabiliwa na shinikizo na kujitenga na rais huyo na kuanzisha hatua ya kumuondoa madarakani.

Siku nane tu kabla ya kumalizika kwa muhula wake, na karibu wiki moja baada ya tukio la uvamizi dhidi ya majengo ya bunge ambayo yanatazamwa kama makao ya demokrasia ya taifa hilo, Trump anakwenda mjini Texas Jumanne hii, katika moja ya ziara zake za mwisho akiwa rais, kupigia chapuo mafanikio ya utawala wake.

Soma pia: Kura ya kumuondoa uongozini Trump kufanyika Jumatano

Mjini Washington lakini, Trump ni mlengwa wa juhudi za kumuondoa madarakani, ikiwemi mchakato wa pili wa kihitoria wa kumshtaki, mara hii kwa uchochezi wa uasi, kuhusiana na uvamizi hatari wa wafuasi wake wa jengo la bunge.

Wafuasi wa Trump walipovamia bunge Januari 6, 2021.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Kwanza, Baraza la wawakilishi litapigia kura hii leo, muswada wa kumtaka Pence na baraza la mawaziri kutumia kifungu cha 25 cha marekebisho ya katiba ya Marekani, ambacho kinaweza kumtangaza Trump kutokuwa na uwezo tena wa kutekeleza majukumu yake na kumuweka Pence kama kaimu rais. Hata hivyo mkutano wa Pence na Trump ulionekana kuondoa uwezekano wa matokeo hayo.

Wawili hao walisisitiza kwamba waliovunja sheria na kuvamia bunge wiki iliyopita hawawakilishi vuguvugu la Amerika Kwanza linaloungwa mkono na Wamarekani milioni 75, na kwa mujibu wa afisa huyo wa juu, wameahidi kuendelea kufanya kazi pamoja kwa niaba ya nchi kwa kipindi kilichobakia katika muhula wao.

Soma pia: Maoni: Kumfungia Trump mitandao ya kijamii haitoshi

Kisha Wademocrat watafuatia kwa mchakato wa kumshtaki Trump, ikiwemo kura ya baraza inayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatano.

Hatua hiyo, ambayo inatishia kuuzika mustakabali wa kisiasa wa Trump -- inaweza kuhitimisha miaka minne ya utata kabla ya kuapishwa kwa Joe Biden hapo Januari 20.

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

01:59

This browser does not support the video element.

Hofu ya vurugu wakati wa uapishwaji wa Biden

Wakati timu ya mpito ya Biden imeelezea imani katika uwezo wa shughuli ya amani ya upaishwaji, idara ya upelelezi wa ndani FBI ilionya kwamba waandamanaji wanaomuunga mkono Trump wanaweza kuvuruga shughuli hiyo.

Idara hiyo, kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha ABC News, pia ilipokea taarifa kuhusu kundi linalotaka kuvamia ofisi za serikali katika majimbo yote 50 siku ya kuapishwa kwa rais mpya.

Maafisa bado wanaendelea na msako wa watu walioshiriki uvamizi wa Capitol baada ya mkutano wa rais Trump, wakati aliporejea madai yake ya uongo kwa Wademocrat walishinda uchaguzi kupitia njia za udanganyifu. Mzingiro huo wa bunge ulisababisha vifo vya watu watano.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW