Trump: Tutaishambulia Iran wasipoifungua njia ya Hormuz
6 Aprili 2026
Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kutoa vitisho vya kuishambulia vikali miundombinu muhimu ya Iran ikiwa serikali ya nchi hiyo haitaufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz ifikapo tarehe yake ya mwisho aliyoitoa ambayo ni hivi leo Jumatatu.
Taarifa hiyo ya Trump inakuja saa chache baada ya mwanajeshi wa pili wa Marekani kuokolewa nchini Iran. Mwanajeshi huyo alipotea wakati Iran ilipoidungua ndege ya Marekani yaF-15E Strike Eagle siku ya Ijumaa.
Iran kwa upande wake nayo imetishia kulenga miundombinu inayohusishwa na Marekani katika ukanda wa mashariki ya kati ikiwa Marekani itaendelea na vitisho vyake.
Vita hivyo vilivyoanzishwa kwa pamoja na Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28 vimeua maelfu ya watu, vimetikisa masoko ya kimataifa, vimekata njia muhimu za meli na kupandisha maradufu bei ya mafuta duniani.