1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump yauweka njiapanda mkutano wa mazingira

10 Mei 2017

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi unaoendelea mjini Bonn unajikuta njiapanda, baada ya Marekani kuahirisha uamuzi wake kuhusu nafasi yake katika Mkataba wa Kimataifa wa Paris.

UNO Bonn
Picha: DW/I. Quaile

Macho yote ya washiriki katika mkutano huo wa siku kumi unaoendelea mjini Bonn hapo jana yalielekezwa mjini Washington, ambako Rais Donald Trump wa Marekani alitarajiwa kukutana na washauri wake, na kisha kutangaza iwapo Marekani inabaki au inajiondoa katika mkataba wa Paris. Lakini baadaye msemaji wa Ikulu ya White House Sean Spicer alithibitishwa kuwa mkutano huo umeahirishwa.

'Kuhusu Mkataba wa ulinzi wa mazingira wa Paris, rais amekuwa akijadiliana na washauri wake kwa muda kuhusu suala hilo, na hatafanya uamuzi wowote kuhusu mkataba huo hadi atakaporudi kutoka mkutano wa G7',  Alisema Spicer.

Mkutano huo wa G7 anaouzungumzia Spicer, utamalizika tarehe 27 mwezi Mei katika mji wa Sicily nchini Italia.

Kunaripotiwa mgawanyiko mkubwa wa maoni miongoni mwa washauri wa Rais Trump kuhusu msimamo wa Marekani juu ya Mkataba wa Paris, ambao ni pamoja na waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson, afisa mkuu ahusikaye na masuala ya kimkakati Steve Bannon na mkuu wa kitengo cha ulinzi wa mazingira katika utawala wa Rais Donald Trump, Scott Pruitt.

''Dhihaka na njama ya China''

Rais Donald Trump anayaita mabadiliko ya tabianchi kuwa dhihakaPicha: Reuters/J. Ernst

Ingawa wakati wa kampeni yake Trump aliahidi kuiondoa mara moja Marekani katika mkataba huo anaoutaja kuwa ''dhihaka na njama ya China dhidi ya Marekani'', rais huyo amelipa jukumu kundi la washauri wake kuunda sera ya nchi kuelekea mkataba huo.

Katika mkutano huu wa Bonn, wataalamu wanapaswa kuandika kanuni zitakazofuatwa katika mchakato wa kupunguza ongezeko la joto duniani, ili lisizidi nyuzi 2 za sentigredi juu ya kiwango kilichokuwepo kabla ya mapinduzi ya viwanda. Sasa hali ya sintofahamu kutoka upande wa Marekani, ambayo ni mchafuzi wa mazingira namba mbili duniani baada ya China, inaughubika mkutano huo, na kuukosesha mwelekeo mchakato mzima.

Huku hali hiyo ikijiri, rais wa China Xi Jinping ambaye pamoja na aliyekuwa rais wa Marekani Barack Obama walisaidia kufikiwa kwa mkataba wa Paris, amesema katika mazungumzo yake na rais mteule wa Ufaransa Emmanuel Macron, kuwa China na Ufaransa zitafanya kazi bega kwa bega kuhakikisha kuwa malengo ya mkataba huo yanafikiwa.

Sintofahamu mjini Bonn

Mkutano huu wa Bonn unalenga kuweka kanuni za utekelezwaji wa mpango wa kupunguza utoaji wa gesi chafuPicha: Getty Images/K. Frayer

Katika chumba cha mkutano hapa mjini Bonn, wazungumzaji wote walipinga vikali hoja ya waziri wa nishati wa Marekani Rick Perry, kutaka mkataba huo ujadiliwe upya.

Marekani imepeleka ujumbe katika mkutano huo, ukiongozwa na Trigg Talley, ambaye aliongoza timu ya Rais Obama wakati mkataba huo wa Paris ulipokuwa ukijadiliwa. Hata hivyo alipoulizwa kutoa maoni na shirika la habari la AFP, afisa huyo wa Marekani alijizuia kusema chochote.

Hatari ya kujiondoa kwa Marekani katika mkataba huo sio tu kwamba inahusu kukwamisha majukumu yake katika kupunguza utoaji wa gesi chafu, lakini pia inaweza kukwamisha juhudi za mataifa yanayoinukia, ambayo katika mchakato huo yanategemea fedha za wahisani, ikiwemo Marekani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga