1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Truss aahidi kuiongoza Uingereza kutoka kipindi kigumu

5 Oktoba 2022

Waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss ameahidi kuiongoza Uingereza kutoka kipindi kigumu cha kiuchumi inachopitia na kutoa mwelekeo wa ukuaji wa uchumi.

Liz Truss visit to US for the United Nations General Assembly
Picha: Stefan Rousseau/REUTERS

Mwezi mmoja baada ya Truss kumrithi Boris Johnson kama waziri mkuu wa Uingereza, amewatenga wapiga kura, masoko ya kifedha na wafuasi wengi katika chama tawala cha Conservative kwa mpango wa haraka wa punguzo la ushuru lililochochewa na madeni ili kukuza uchumi uliodumaa wa Uingereza. Lakini katika hotuba yake ya Jumatano (05.10.2022), Truss amesema kuwa hali kubaki jinsi ilivyo sio suala la chaguo licha ya kukwama mpango wake wa kifedha na kusababisha kubatilisha ahadi ya kupunguza kodi ya mapato kwa watu wa kipato cha juu zaidi.

Truss anasema Uingereza inahitaji kujiimarisha

Truss amewaambia wajumbe katika kongamano hilo kwamba katika nyakati hizi ngumu, wanahitaji kujiimarisha na kukosoa kile alichokitaja kuwa "Muungano unaopinga ukuaji" unaozuia juhudi za kufufua uchumi. Truss ameongeza kusema wanahitaji kupiga hatua na kwamba kama wiki chache zilizopita zilivyoonesha, itakuwa ngumu. Truss pia amesema, wakati wowote kuna mabadiliko, kuna usumbufu na sio kila mtu atapendelea mabadiliko, lakini kila mtu atafaidika kutokana na matokeo ambayo niuUchumi unaokua na maisha bora ya baadaye.

Wakati wa hotuba hiyo, Truss pia amesema kwamba waziri wa fedha na gavana wa Benki ya Ulaya wataendelea kuratibu kwa karibu sera za kifedha na kwamba yeye na waziri huyo wanakubaliana kabisa kuhusu suala hilo.

Kwasi Kwarteng - Waziri wa fedha wa UingerezaPicha: Justin Ng/Avalon/Photoshot/picture alliance

Waziri wa zamani Grant Shapps, ambaye alimuunga mkono mpinzani wa Truss Rishi Sunak, ameiambia redio ya Times kwamba Truss anaweza kukabiliwa na kura ya wabunge ya kutokuwa na imani naye ikiwa hotuba hiyo kuu itashindwa kuanza kuubadilisha mtizamo mbaya wa chama hicho katika kura za maoni.

Wanaharakati wa Greenpeace watatiza utoaji wa hotuba

Awali waandamanaji wawili wa shirika la mazingira la Greenpeace Rebecca Newsom and Ami McCarthy waliokuwa miongoni mwa washirika wa kongamano hilo mjini Birmingham, walitatiza kwa muda mfupi hotuba hiyo ya waziri mkuu na kuanza kupiga kelele huku wakipeperusha bendera ya manjano iliyokuwa imeandikwa ''nani alipigia kura hili?'' huku pia ikiwa na nembo ya shirika hilo.

Shirika la Greenpeace lilithibitisha kupitia mtandao wa twitter kwamba wanaharakati wake walitatiza hotuba hiyo, kumtuhumu waziri huyo mkuu kwa kuzivunja kabisa ahadi za ilani ya chama hicho ya mwaka wa 2019.

Mwezi uliopita, serikali ya Truss iliondoa marufuku ya muda dhidi ya aina ya uchimbaji unaotumika kutafuta mafuta au gesi asilia kutoka kwenye kina kirefu chini ya ardhi ambao umekuwa ukitumika tangu mwaka 2019 na kusema kuimarisha usambazaji wa nishati lilikuwa suala la kipaumbele kabisa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW