1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Truss ajiuzulu baada ya wiki sita kama waziri mkuu Uingereza

20 Oktoba 2022

Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss amejiuzulu Alhamis, wiki sita tu baada ya kuchukuwa wadhifa huo, licha ya kusisitiza siku moja kabla kuwa haendi kokote. Mrithi wa Truss anatarajiwa kuchaguliwa kufukia Oktoba 28.

Liz Truss UK Rücktritt
Picha: TOBY MELVILLE/REUTERS

Katika tamko lililoandaliwa haraka nje ya ofisi yake Mtaa wa Downing, Truss amekiri kwamba hawezi kutekeleza mamlaka aliopewa na chama chake cha Conservative, lakini amesema atabakia kuwa waziri mkuu hadi mrithi wake atakapochaguliwa wiki ijayo.

Truss ndiye waziri mkuu wa tatu wa Conservative kujiuzulu katika miaka michache na amekiacha chama hicho kilichogawika kikitafuta kiongozi anaeweza kuunganisha makundi yake yanayolumbana. Truss amekuwa waziri mkuu wa siku 45 tu.

Wahafidhina waliogawika vibaya wana siku chache tu kukubaliana juu ya mrithi wa Truss, au wakabiliwe na mchuano mwingine wa uongozi, wa tatu katika muda miaka mitatu.

Wanaotizamiwa kuwania wadhifa huo ni waziri wa zamani wa fedha Rishi Sunak, alieshindwa na Truss katika kinyang'anyiro kilichopita, kiongozi wa bunge la wawakilisi Penny Mordaunt, waziri wa ulinzi Ben Wallace, na Boris Johnson, waziri mkuu wa zamani alieondolewa mwezi Julai kufuatia mkururo wa kashfa.

Liz Truss amekaa madarakani kwa siku 45 tu.Picha: Alberto Pezzali/AP Photo/picture alliance

Truss alitupa daruga siku moja tu baada ya kuapa kusalia madarakani, akisema alikuwa "mpiganaji na siyo mkataji tamaa." Lakini ameshindwa kuendelea baada ya waziri mwandamizi kuondoka serikalini huku akimkosoa vikali, na kura katika bunge kuishia katika machafuko na mapambano, siku chache tu baada ya kulaazimika kuachana na nyingi kati ya sera zake za kiuchumi.

Masoko yamevuta pumzi na sarafu ya pauni kuongezeka thamani kwa karibu asilimia moja na kuzidi $1.3 baada ya kujiuzulu kwa Truss.

Soma zaidi: Uingereza: Mivutano yazidi kuudidimiza uongozi wa Waziri Mkuu Liz Truss

Idadi inayoongezeka ya wabunge wa Conservative walimtolea wito Truss kuachia ngazi baada ya wiki ya machafuko yaliosababishwa na mpango wake wa kiuchumi wa Septemba 23, ambao ulihusisha makato kadhaa ya kodi yaliosababisha mtikisiko katika masoko ya fedha, ambao wawekezaji walielezea wasiwasi kwamba Uingereza isingeumudu.

Labour yataka uchaguzi mpya

Kiongozi wa chama cha Labour Keir Starmer, ambaye chama chake cha upinzani kimeshuhudia uungwaji wake mkono ukiongezeka pakubwa katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura kufuatia muhula mfupi wa Truss uliokumbwa na mzozo, ametaka uchaguzi mkuu uitishwe "sasa."

"Tuko tayari kuunda serikali ili kutuliza uchumi na kutekeleza mpango halisi wa ukuaji, wa kuboresha viwango vya maisha, kusaidia watu kuvuka mzozo wa gharama za maisha. Na hilo ndiyo chaguo sasa: Seriakli imara au vurugu hizi kutoka kwa Wahafidhina," alisema Starmer.

Soma zaidi: Waziri Mkuu Truss asisitiza hang'oki

Mwisho wa Truss umekuja baada ya waziri wa mambo ya ndani Suella Braverman kujiuzulu, na wabunge wengi wa chama cha Conservative kuasi katika vurugu zilizoshuhudiwa bungeni jana usiku.

Kufikia Alhamisi, zaidi ya dazeni moja ya wabunge wa Conservative walitamka hadharani Truss ajiuzulu, na wengine zaidi waliripotiwa kuwasilisha barua kwa Brady wakitaka aondolewe, ingawa sheria za chama zimepiga marufuku kampeni nyingine ya uongozi kwa muda wa miezi 12.

Mwenyekiti wa Kamati ya wabunge wa Conservative inayohusika na uchaguzi wa viongozi Grahma Brady, ametangaza kinyang'anyiro cha kumchagua mrithi wa Truss kitafanyika kufikia Oktoba 28.

Kulingana na chama cha Conservative, kura za kwanza za wabunge zitapigwa siku ya Jumatatu katika saa tisa na kumi na moja jioni, na endapo kutakuwa na haja ya duru ya pili, itafanyika kati ya saa 11 na saa mbili jioni.

Soma zaidi: Truss aomba radhi kwa makosa lakini hatazamii kujiuzulu

Madhila ya waziri Mkuu huyo yalianza wakati mpango wake wa kupunguza kodi, uliposababisha sokomoko kwenye masoko ya fedha ambalo lilitishia mifuko ya pensheni, na kumlaazimisha kufanya mabadiliko kadhaa ya kufedhesha.

Kuondoka kwa Braverman Jumatano, kulisababisha mabadiliko ya pili ya baraza la mawaziri mwezi huu, baada ya hapo awali Truss kumfuta kazi mshirika wa karibu Kwasi Kwarteng kuhusiana na vurumai la bajeti, na nafasi yake kujazwa na Jeremy Hunt, ambaye mara moja alifuta karibu matangazo yote ya kisera.

Chanzo: Mashirika