Tsai:Mazoezi ya jeshi la China yaondoa utulivu wa kikanda
11 Aprili 2023Kupitia ukurasa wake wa Facebook rais Tsai ameandika, kama rais anawakilisha taifa lake duniani na ziara zake nje ya nchi ikiwemo Marekani si jambo geni na kuongeza kwamba China ilitumia mwanya huo kuanzisha mazoezi ya kijeshi hatua ilioondoa utulivu kwa Taiwan na kanda kwa ujumla wake.
Matamshi hayo ameyatoa wakati China tayari imemaliza mazoezi yake ya kijeshi ya siku tatu yaliopewa jina la "upanga wa Pamoja" ikiyataja yenye mafanikio makubwa.
Soma pia:China yahitimisha luteka za kijeshi kuizunguka Taiwan
Hapo awali wizara ya Ulinzi ya kisiwa hicho ilisema ilibaini kuwepo kwa meli 12 za kivita za China pamoja na ndege 91 siku ya Jumatatu.
Wizara hiyo ilisema ndege ya kivita chapa J15 iliruka kutoka meli ya Shandong na ilikuwa mojawapo kati ya ndege 54 zilizovuuka mpaka na kuingia anga ya Taiwan.
China na mshirika wake Urusi watetea luteka hizo
Taarifa iliyotolewa na Kamandi ya Mashariki ya Jeshi la Ukombizi wa Watu, PLA, ilisema "mazoezi hayo yalijaribu kwa kina uwezo wa pamoja wa matawi ya kijeshi kushambulia kwenye mazingira halisi."
Taarifa hiyo iliongeza kwamba wanajeshi wa China walikuwa "tayari kwa mapambano na wanaweza kupigana wakati wowote, na watakabili kwa nguvu zote "namna yoyote ya hisia za kujitenga kwa Taiwan na majaribio ya uingiliaji kati wa kigeni."
Soma pia:Taiwan yabain ndege za kivita 59 na meli 11 za China
Mshirika wa karibu wa China, Urusi, ilitetea mazoezi hayo ya kijeshi, huku msemaji wa Ikulu ya Kremlin alisema "Beijing ina haki ya kulinda mamlaka yake na kujibu matendo ya uchokozi."
China ambayoiliionya Marekani kumruhusu Tsai kukutana na Spika wa Bunge Kelvin McCarthy haijasita kufikiria kutumia nguvu kukirudisha Kisiwa hicho kinachojitawala kidemocrasia chini ya udhibiti wa Beijing.