1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi aahidi kupambana na waasi wa ADF

John Kanyunyu18 Juni 2021

Rais Félix Tshisekedi amekamilisha ziara yake katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini. Kabla ya kuondoka Beni, Tshisekedi alifanya mazungumzo na wajumbe mbalimbali wa kijamii wakiwemo wanafunzi.

DR Kongo Goma | Besuch Präsident Felix Tshisekedi
Picha: Giscard Kusema

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi amekamilisha ziara yake katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini hasa katika eneo la Beni na Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kabla ya kuondoka Beni, Tshisekedi alikutana kwa mazungumzo na wajumbe mbalimbali wa kijamii, miongoni mwao wanafunzi. 

Rais Félix Antoine Tshisekedi alidondokwa na machozi, alipokuwa anazungumza na mwanafunzi Jason Kahiwa, mjumbe wa wanafunzi ambao siku zilizopita waliwahi kupiga kambi kwenyi ofisi ya Meya wa Beni kumuomba rais aje hapa kuleta suluhu ya kudumu, ili kusimamisha mauwaji.

Jason Kahiwa ndiye pia spika wa bunge la watoto wa Beni amesema, "Fimbo tulizochapwa, kutupwa kwetu jela, haki ambayo hatukutendea sisi zisiwe tu za kuwagandamiza wananchi, bali zikupatie nguvu na juhudi ili amani irudi kwetu. Ndio haja ya msingi. Amani."

Soma zaidi: Bunge DRC laongeza muda wa hali ya dharura mikoa ya mashariki

Akipigwa na butwaa, baada ya kupata taarifa kamili ya dhulma waliyofanyiwa wanafunzi na vyombo vya dola, wakati wanafunzi hao wakifurushwa kutoka ofisi ya Meya, Rais Tshisekedi amewaahidi kwamba patafanyiwa na uchunguzi na waliowachapa viboko wanafunzi hao wataadhibiwa na wale pia walioleta taarifa za uongo kwake kuhusu wanafunzi hao, "Kwa niaba ya waliowateseni, nawaomba msamaha. Msamaha huo unatoka moyoni mwangu. Na sikuwa na taarifa kuhusu unyama huo dhidi ya watoto, lakini nadhani kwamba uchunguzi unapaswa kufanyika ili wahusika waadhibiwe."

Matamshi haya ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanaonekana kuwapanguza majonzi baadhi ya wakaazi wa Beni, waliokuwa wanadhani kwamba Rais Tshisekedi ameshawapa kisogo.

Baada ya Beni, Rais Tshisekedi aliuzuru mji wa kibiashara wa Butembo, ambako aliwahutubia wakaazi waliokuja kumlaki kwenye njia kuu ya mji huo.

Je, kiswahili cha Congo kina mapungufu?

02:16

This browser does not support the video element.

Katika hotuba yake, Rais huyo aliwatumia ujumbe mkali waasi wa ADF, akiwataka kuachana na kuwauwa wa Congo, huku akiapa kupambana nao hadi mwisho, "Nakuja kuwaambia maadui zetu, maadui wa nchi, hao wanaoitwa ADF waache kuwauwa watoto wa Congo. Tutapambana nao hadi mwisho na hatutachoka kamwe. Wakifiri kwamba watatushinda wanajidanganya."
 

Kabla ya kuondoka katika eneo hili na kwenda Bunia, mji mkuu wa mkoa wa Ituri, Rais Tshisekedi alikutana pia kwa mazungumzo na viongozi wa kijeshi, aliowataka wafanye kazi haraka iwezekanavyo, ili amani ya kudumu irudi katika eneo hili la mashariki ya Congo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW