1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi aiandama Rwanda Umoja wa Mataifa

21 Septemba 2022

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametumia hotuba yake kwenye Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa kuituhumu moja kwa moja Rwanda kwa kulisaidia kundi la waasi la M23 mashariki mwa nchi yake.

Felix Tshisekedi und Paul Kagame | Präsidenten DR Kongo und Ruanda
Picha: SIMON WOHLFAHRT/AFP/Getty Images

Ilikuwa ni saa 8:00 usiku wa kuamkia Jumatano (Septemba 21) kwa majira ya Afrika Mashariki, wakati Rais Tshisekedi alipopanda kwenye kiriri cha Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa katika kile wachambuzi wa hotuba za viongozi wanachokiita "muda wa mashitaka."

Sehemu kubwa ya hotuba yakeilijikita kwenye kuelezea jinsi ukosefu wa usalamaunavyoendelea kuiadhibu nchi yake kwa miongo kadhaa sasa, akifananisha mifumo na makubaliano yote ya kurejesha amani kama jengo lililojengwa juu ya msingi mbovu na hivyo kutokuwa na budi ya kuporomoka.

Soma pia:MONUSCO:Haipo tayari kukabiliana na M23

Tshisekedi alisema Wakongo wameshachoka na hali hii inayojirejea miaka nenda miaka rudi na sasa wanataka uthabiti na udhibiti kamili ya nchi yao.

Rais wa DCR Felix Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda

"Sisi, watu wa Kongo, sasa tumedhamiria kukomesha moja kwa moja hali ya ukosefu wa usalama  mashariki mwa nchi yetu kwa gharama yoyote ile.

Muda umefika wa kuvunja moja kwa moja mduara wa papo kwa papo wamachafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuliweka eneo la Maziwa Makuu kwenye uthabiti, ili kufaidika na fursa zake za kiuchumi kadiri inavyowezekana na utajiri wake wa baianuwai ili kuwaokowa wanaadamu dhidi ya janga la mabadiliko ya tabianchi." Alisema Tshisekedi.

Akiinyooshea kidole mara kwa mara Rwanda  rais huyo wa Kongo alisisitiza jukumu la taifa hilo jirani kwenye msiba unaowakumba Wakongo kwenye maeneo ambayo jeshi la Rwanda na wapiganaji wa M23 wanakutikana mashariki mwa Kongo. 

Kuwajibishwa Rwanda?

Kwa mujibu wa Kinshasa, M23 ni washirika wa Kigali na Tshisekedi alitumia ripoti kadhaa za Umoja wa Mataifa kuthibitisha tuhuma zake hizo, akisema kwamba suala la kuhusika kwa Rwanda kwenye uungaji mkono wake kwa M23 si jambo tena la kubishaniwa.

Kiongozi huyo wa Kongo aliutaka Umoja wa Mataifa kuongeza shinikizo lake dhidi ya Rwanda na M23 ambayo viongozi wake wamewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa,kwa lengo la kuifanya Rwanda kukoma kuliunga mkono kundi hilo la waasi na kuanza mara moja kutekeleza makubaliano yaliyomo kwenye  Mkataba wa Luanda.

Soma pia:Viongozi wa DR Congo na Rwanda kufanya mazungumzo nchini Angola

Vile vile alitowa wito wa kuendelezwa kwa mchakato wa amani wa Nairobi na kutumwa kwa kikosi cha walinda amani kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki kusaidia kurejesha utulivu mashariki mwa Kongo.

Kwa upande mwengine, Tshisekedi alikanusha tuhuma zinazotolewa na Rwanda kwamba Kongo inawapa hifadhi waasi wa kundi FDLR ndani ya mipaka yake.

Kwa upande wa nafasi ya Kongo kilimwengu, Tshisekedi alihoji kwamba nchi yake ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa madini ya kimkakati kuelekea kwenye matumizi mbadala ya nishati na kuondosha utoaji gesi chafu kwenye sekta ya usafiri. 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW