Tshisekedi aidhinisha jeshi la Uganda kuingia Congo
29 Novemba 2021Mwito huo umejitokeza baada ya baadhi ya duru kujulisha kwamba Rais Félix Tshisekedi tayari ameidhinisha jeshi la Uganda kuvuka mpaka, ili kupambana na waasi wa ADF wanaolaumiwa kuwaua raia huko mashariki ya Kongo.
Hadi sasa halijatolewa tangazo rasmi kutoka Kinshasa au Kampala, lakini ni Bunge la taifa ndilo liliwahi kupendekeza kwa serikali kuunganishwa vikosi hivyo viwili.
soma Mashambulizi mashariki mwa Congo yaendelea kutesa raia
Lengo ni kuimarisha majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) ambayo yanapambana na waasi wa ADF katika eneo la mashariki mwa Kongo, kama alivyoeleza mubunge Bertin Mubonzi, ambaye anaongoza tume ya ulinzi na usalama katika Bunge la Kitaifa.
Miongoni mwa mapendekezo yetu kwa serikali, kulikuwa na kuunganisha vikosi kama inavyofanyika katika nchi zote za ulimwengu. Kuunganisha jeshi letu na lile la nchi rafiki ili kuimarisha majeshi, kutasaidia kumaliza vita huko mashariki. Tumetoa mapendekezo, sasa ni dhamu ya serikali kuamua. Zaidi ya hayo, tusubiri mambo yawe rasmi.
Wakongomani wengi bado wanazo kumbukumbu mbaya za mkusanyiko wa vikosi, baada ya majeshi ya Rwanda na Uganda kupambana mwaka 2000 huko Kisangani, mji ulio na madini katika sehemu ya kaskazini-mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.
Halafu chama cha demokrasia na mageuzi ya kweli (MDVC) kimeonya kwamba ni uporaji wa utajiri wa Kongo ndio unalengwa. Justin Mudekereza, kiongozi wa chama hicho cha upinzani ameonya dhidi ya mpango wa kuigawa nchi hii na hivyo katoa mwito kwa Wakongomani kuzuia idhini ya wanajeshi wa Uganda kwenye eneo la Kongo.
Kwa kuzuwia mbinu ya mpango wa kuigawa nchi yetu na ule wa kupora rasilimali zetu unaoendelea, huku wanainchi wakiishi katika hali ya umaskini, nawaalika Wakongomani wote wasimame kama mtu mmoja ili kulizuia Bunge lisiidhinishe mchezo huo wa usaliti wa hali ya juu.
Ni tangu Mei ndiyo Ituri na Kivu Kaskazini zimezingirwa ili kukomesha ghasia katika mikoa hiyo miwili. Lakini hadi leo, matokeo bado siyo ya kuridhisha.
Jean Noël Ba-Mweze, DW, Kinshasa.