1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi aitaka MONUSCO kuondoka haraka Kongo

21 Septemba 2023

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alhamisi unaingia siku yake ya tatu jijini New York, Marekani, ambapo viongozi mbalimbali wanatarajia kuendelea kuhutubia pamoja na kufanyika mikutano ya pembezoni.

UN Vollversammlung | Felix-Antoine Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Felix TshisekediPicha: Leonardo Munoz/AFP/Getty Images

Katika kikao cha Jumatano, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Tshisekedi alitoa wito wa kuondolewa haraka kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO.

Akihutubia katika mkutano huo, Rais Tshisekedi alisema kikosi hicho ambacho kimekuwepo Kongo kwa takribani miaka 25 na chenye askari 15,000 kimeshindwa kukabiliana na makundi yenye silaha, kuwalinda raia, na hata kurejesha amani nchini humo, na kwamba ni sawa na kuendelea kujidanganya kung’ang’ania kiendelee kudumisha amani.

Serikali kuanza mazungumzo na Umoja wa Mataifa

Alisema ameiagiza serikali yake kuanza mazungumzo na maafisa wa Umoja wa Mataifa, ili kuhakikisha inaharakisha zoezi la kuondoka kwa MONUSCO nchini Kongo, na kubadili muda wa mwisho wa kuondoka kwa kikosi hicho kutoka Desemba 2024, hadi Desemba 2023.

"Kufuatia uwepo wa zaidi ya miongo miwili na Umoja wa Mataifa, ni wakati muafaka wa nchi yangu kuchukua udhibiti kamili na kuangalia hatma yake, na kuwa mstari wa mbele katika kuleta utulivu wake," alisisitiza Tshisekedi.

Kiongozi huyo wa Kongo alisema wanaishukuru jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kwa msaada wao na ushirikiano wao, lakini wanafahamu pia kwamba kujiondoa kwa MONUSCO kwa awamu ni hatua muhimu ya kuleta maendeleo ambayo tayari wameshayapata.

Kifaru cha MONUSCO kikiwa Kivu Kaskazini, KongoPicha: Djaffar Sabiti/REUTERS

Kwa miaka kadhaa sasa, suala la kuondoka kwa MONUSCO limekuwa kiini cha mijadala na mivutano hasa kuhusu mustakabali wa Kongo.

Katika mkutano wa mwezi Juni wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani ilionya kuhusu kuondolewa haraka kwa MONUSCO, ikisema kuwa Kongo haiko tayari kuachana na askari hao ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023.

Kwa upande mwingine Tshisekedi pia alitoa wito wa kuongezwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuhakikisha kuna wawakilishi wawili kutoka katika bara la Afrika, kama wanachama wa kudumu.

Kenya na Haiti zaanzisha uhusiano wa kidiplomasia 

Wakati huo huo, Kenya na Haiti zimeanzisha uhusiano wa kidiplomasia, wakati ambapo kuna mazungumzo ya kimataifa kuhusu uwezekano wa Kenya kuongoza kikosi kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kulisaidia jeshi la polisi kupambana na kuongezeka kwa vita vya magenge ya Haiti.

Akizungumza Jumatano katika hafla ya kuanzishwa kwa balozi hizo, iliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Rais wa Kenya, William Ruto alisema nchi yake ina nia thabiti ya kuongoza kikosi hicho kupambana na magenge hayo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry, ambaye mwaka mmoja uliopita alitoa wito wa kupelekwa haraka kikosi kama hicho nchini Haiti.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni Picha: Eduardo Munoz/REUTERS

Aidha, Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni ameutaka Umoja wa Mataifa kuanzisha "vita ya kimataifa bila ya huruma" dhidi ya watu wanaofanya biashara ya wahamiaji, baada ya kuongezeka kwa wahamiaji wanaowasili kwenye kisiwa cha Lampedusa.

"Italia iko tayari kuongoza juhudi dhidi ya wafanyabiashara hao wa utumwa," alisema Meloni wakati akihutubia katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York.

Iran yaishutumu Saudia kwa usaliti

Naye Rais wa Iran, Ebrahim Raisi ameishutumu Saudi Arabia kwa kuwasaliti Wapalestina, kutokana na harakati zake za kurejesha uhusiano na Israel. Raisi amesema wanaamini kuwa uhusiano kati ya nchi za kikanda na utawala wa Israel utakuwa usaliti kwa watu wa Palestina.

Viongozi wanaotarajiwa kuhutubia Alhamisi ni Rais wa William Ruto wa Kenya, Makamu wa Rais wa China Han Zheng, Kiongozi wa kijeshi wa Sudan Abdel-Fattah Burhan, kiongozi wa serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa Rashad al-Alimi, na Rais wa Sri Lanka, Ranil Wickremesinghe.

Wengine watakaohutubia katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, pamoja na Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas.

(AFP, AP, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW