Tshisekedi akubali kukutana na Kagame
28 Februari 2024Kufuatia mkutano wa ana kwa ana wa masaa matatu mjini Luanda, Angola, Rais Felix Tshisekedi na mwenyeji wake Joao Lourenco hawakutoa kauli yoyote mbele ya waandishi habari. Lakini waziri wa mambo ya nje wa Angola, Tete Antonio amesema Tshisekedi amekubali kuzungumza na mwenzake Paul Kagame wa Rwanda.
''Matokeo ya mkutano huu ni kwamba rais Tshisekedi amekubali kimsingi kukutana na rais wa Rwanda, Paul Kagame. Na Angola kama mpatanishi sasa ina jukumu kufanya kazi ili kufanikisha mkutano huo.'', alisema Tete.
Mkutano huu kati ya Tshisekedi na Lourenco unafuatia mkutano mdogo ulioandaliwa Februari 18,pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia. Lengo kuu hivi sasa kwa rais wa Angola ni kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya marais wa Kongo na Rwanda ili kumaliza vita huko Kivu ya Kaskazini.
''Kusitishwa haraka kwa mapigano''
Hatua ya Tshisekedi kukubali mazungumzo na Kagame imekuja miezi mitatu baada ya kiongozi huyo kuapa kwamba hawezi tena kukutana na jirani yake huyo hadi mbele ya Mungu. Hata hivyo, Ikulu ya Kongo tayari imetoa masharti kabla ya mkutano wowote baina ya Tshisekedi na Kagame. Ikiwemo kuondolewa mara moja kwa wanajeshi wa Rwanda katika eneo la Kongo. Giscard Kusema, ni afisa wa mawasiliano ya Ikulu ya Kongo.
''Msimamo wa rais Tshisekedi ni wazi. Mkutano na Kagame unawezekana endapo vikosi vya Rwanda vya RDF vitaondoka mara moja nchini Kongo, kusitishwa haraka kwa mapigano na kupokonywa silaha kwa kundi la kigaidi la M23.'', alisisitiza Kusema.
Idara ya mawasiliano ya rais wa Kongo pia inabainisha kuwa hakuna tarehe au eneo ambalo limepangwa kwa ajili ya mkutano huo iwapo utafanyika. Rais wa Angola ambaye ni mpatanishi wa mzozo baina Kongo na Rwanda anatarajiwa pia kukutana na Rais wa Rwanda.
Monusco yaanza kuondoka Kongo
Huku hayo ya kijiri, Ujumbe wa Umoja wa mataifa wa kulinda amani nchini Kongo Monusco, umeanza hii leo zoezi rasmi la kuondoka nchini humo. Maafisa wa MONUSCO wanatarajiwa kukabidhi kituo cha kwanza cha Umoja wa Mataifa kwa polisi wa kongo. Zoezi hilo litafanyika mjini Kamanyola jimboni Kivu ya Kusini.
Serikali na wananchi wa Kongo wamekuwa wakikituhumu hikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kutokuwa na ufanisi katika kuwalinda raia dhidi ya makundi yenye silaha.