Tshisekedi atimiza miaka 4 madarakani
24 Januari 2023Wakati wafuasi wake wakijivunia tathmini yake ambayo wanaielezea kuwa chanya kwa kiasi kikubwa, wanaamini kwamba anastahili muhula wa pili, huku upinzani na mashirika ya kiraia vinazungumzia Tshisekedikushindwa kwenyi ngazi zote.
Chama cha UDPS cha Rais Félix Tshisekedi pamoja na muungano wa vyama vinavyomuunga mkono kwa ujumla, vinajivunia mafanikio yake vikiamini kwamba tathmini yake inakidhi mahitaji mengi ya Wakongo, kama alivyoeleza Ntumba Tshabola Bintu, mbunge wa UDPS.
"Rais wa Jamhuri anataka kutimiza ahadi zake kwa Wakongo, ndiyo maana alianza kuruhusu Jamhuri kuwa na uwezo. Alikuta bajeti ya bilioni nne ambayo 60% kutoka nje ya nchi. Leo tuna bajeti ya dola bilioni 16. Kuhusu nyanja ya kijamii, rais anaishughulukia na anatumika kwa umakini."
SOMA PIA: Upinzani wamshutumu Tshisekedi kuanzisha kampeni ya mapema
Mitazamo tofauti
Matamshi hayo yemetupiliwa na upinzani ukiamini kwamba raïs Tshisekediameshindwa kabisa kwani inaonekana wazi, Kongo inarudi nyuma kila siku kutokana na uongozi mbovu. Ndivyo alivyoeleza Ferdinand Kambere, Naibu Katibu Mkuu wa chama cha PPRD, chama cha Rais wa zamani Joseph Kabila.
"Kwenye ngazi ya kisiasa kwa mfano, tume ya uchaguzi haijakuwepo wakati tayari tuko Januari tukianza mwaka wa uchaguzi. Kuhusu usalama hata tusizungumzie kwani idadi kubwa ya wananchi wanatawaliwa na majeshi ya kigeni na hatuoni mpango wa serikali ili kuwaondoa kabla ya uchaguzi."
SOMA PIA: Maandamano Bukavu kumtaka Rais Tshisekedi kuheshimu katiba
Baadhi ya mashirika ya kiraia pia yanaunga mkono kauli hiyo. Vuguvugu la Kupigania Mabadiliko (LUCHA), limekumbusha na kumshutumu rais kwa ahadi nyingi zisizotimizwa, kutekwa nyara mchakato wa uchaguzi pamoja na hali ya usalama kuendelea kuzorota mashariki mwa nchi hii. Bienvenu Matumo ni mwanaharakati wa vuguvugu LUCHA.
"Raïs wa jamhuri aliendelea kuwaahidi Wakongo kama ataboresha hali ya maisha yao, ila baada ya miaka minne hatujaona hali hiyo kuboreshwa. Tulichokitambua ni kwamba matendo ya rais pamoja na serikali yake havijaambatana na ahadi hizo. Tuliona pia akichukua hatua kiholela ambazo ziliharibu hali ya usalama".
Baada ya ushindi wa kutatanisha katika uchaguzi wa Desemba 2018, Félix Tshisekedi alimrithi Joseph Kabila mnamo Januari 24 mwaka 2019 katika makabidhiano ya amani ya mamlaka kwa mara ya kwanza kabisa hapa nchini Kongo.