1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi atoa maneno makali dhidi ya kikosi cha EAC

10 Mei 2023

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amekikosowa vikali kikosi cha wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kilichotumwa kurejesha amani nchini mwake, akisema mwisho wake ni mwezi Juni.

Felix Tshisekedi | Präsident Demokratische Republik Kongo
Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Akizungumza kwenye ziara yake ya siku nne nchini Botswana iliyoanza Jumanne (Mei 9), Rais Tshisekedi alidai kuna "usuhuba" baina ya waasi na kikosi hicho cha mataifa ya EAC kilichotumwa nchini mwake mwaka jana, ambako kuna mamia ya makundi ya waasi.

Makundi hayo ni matokeo ya vita vya kikanda vilivyotawala eneo hilo kwenye miaka ya 1990 na 2000, ingawa kwa sasa ni kundi moja makhsusi la M23 ndilo linalotajwa kuwa na nguvu zaidi kuliko mengine.

Soma zaidi: Hatihati kwa M23 kuondoka kwenye maeneo wanayodhibiti

Kundi hilo kwa haraka lilifanikiwa kuyadhibiti maeneo kadhaa tangu lilipozuka tena mwishoni mwa mwaka 2021 na kuifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye mataifa wanachama saba kuunda kikosi cha kijeshi kukabiliana na hali hiyo mnamo Juni 2022.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania (kulia) alipomkaribisha Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jijini Dar es Salaam mwezi Oktoba 2022. Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa EAC na SADC.Picha: Tanzania State House

Kenya ilikuwa ya kwanza kutuma wanajeshi wake mwezi Novemba, ikifuatiwa na Burundi, Uganda na baadaye Sudan Kusini. 

Tshisekedi ahoji dhamira ya kikosi cha EAC

 "Tumegunduwa kuna usuhuba baina ya kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki na waasi. Hilo ni tatizo kubwa panapohusika jukumu la kikosi hicho na ambalo linatulazimisha tuulize, ni ipi hasa dhamira ya kikosi hiki?" Alihoji Tshisekedi.

Rais huyo wa Kongo aliwaambia waandishi wa habari mjini Gaborone kwamba wanajeshi pekee wanaoonesha tabia tafauti ni wale wa Burundi, lakini waliobakia wote "wanaishi pamoja na waasi wa M23."

Soma zaidi: Usalama wazidi kuzorota nchini Kongo

Kauli hii nzito kwenye uwanja wa diplomasia ilitolewa siku moja tu baada ya kikao maalum cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kilichofanyika nchini Namibia kuamua kutuma kikosi chengine cha wanajeshi "kurejesha amani na usalama mashariki mwa Kongo." 

Ukomo wa kikosi cha EAC ni Juni 2023

Tshisekedi alisema muda wa kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki unafikia ukomo wake mwezi Juni 2023 na kwamba endapo watahisi kuwa jukumu lao hawakulitelekeza, basi "watawarejesha makwao na kuwashukuru kwa kujaribu na nafasi yao itachukuliwa na kikosi cha SADC."

Rais Felix Tshisekedi (kushoto) na Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye nchi yake inatuhumiwa kuliunga mkono kundi la M23 mashariki mwa Kongo.

 

Soma zaidi: Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wawasili DRC

Hata hivyo, siku ya Jumatatu (Mei 8), Rais Hage Geingob wa Namibia alisisitiza haja ya mataifa ya SADC kufanya kazi pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki "ili kuratibu juhudi zao katika kuisadia Kongo."

Mataifa ya SADC yanazijumuisha Afrika Kusini, Angola, Tanzania, Namibia, Zambia, Msumbiji, Zimbabwe na yenyewe Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vyanzo: Reuters, AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW