1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi awasilisha rasmi fomu kuwania urais

8 Oktoba 2023

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amerejesha fomu ya kugombea tena nafasi hiyo kwa muhula wa pili, akijiunga na orodha refu inayojumuisha wanasiasa wakubwa akiwemo mshindi wa Nobel.

Felix Tshisekedi | Präsident Demokratische Republik Kongo
Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Tshisekedi, aliyeingia madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2018, aliwasilisha rasmi fomu za kuwania urais kwa miaka mingine mitano mjini Kinshasa siku ya Jumamosi (Oktoba 7).

Kwa hatua hiyo, anaungana na wagombea wengine zaidi ya kumi, wakiwemo wanasiasa wakubwa na mawaziri wa zamani serikalini, ingawa wengi wanaamini upinzani umekuwa dhaifu sana kutokana na kugawanyika kwake.

Soma zaidi: Tshisekedi aitaka MONUSCO kuondoka haraka Kongo

"Ana fursa nzuri zaidi ya kushinda," alisema mwanasayansi wa siasa wa Kongo, Christian Moleka, alipokuwa akizungumza na shirika la habari la AFP.

"Ni mgombea anayetetea nafasi yake, ana rasilimali na nyenzo za dola, watu bado wanamuamini na amefanikiwa kujenga miungano ya kimkakati," aliongeza msomi huyo.

Upinzani uliogawanyika utahitaji kuungana na kusimamisha mgombea mmoja ili kujipa nafasi ya kumshinda Tshisekedi, kwa mujibu wa Moleka.

Lakini uwezekano wa kufanya hivyo unaonekana kuwa mdogo, kwani wagombea kadhaa wenye nguvu wamejitokeza kila mmoja kivyake.

Utitiri wa wagombea

Moise Katumbi, mfanyabiashara mkubwa na gavana wa zamani wa jimbo la Katanga ni miongoni mwa wanaowania, baada ya mwaka 2018 kuzuiliwa na utawala wa Joseph Kabila kugombea urais kwa madai kuwa baba yake alikuwa raia wa Italia.

Baadhi ya wagombea urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia wa Kongo. Kutoka juu kushoto: mgombea anayetetea kiti chake, Felix Tshisekedi, Moise Katumbi, Denis Mukwege na Martin Fayulu.Picha: AFP/Getty Images, picture alliance, G. Kusema, DW

Kwenye orodha ya wagombea wamo mawaziri wakuu wawili wa zamani, wote waliohudumu chini ya Kabila: Augustin Matata na Adolphe Muzito.

Soma zaidi: Fayulu, Kabila wajitoa uchaguzi DRC

Mwengine ni Noel Tshiani, ambaye aliwania na kushindwa kwenye uchaguzi uliopita. Ni yeye ndiye aliyekuwa mpigachapuo mkubwa wa sheria inayotaka wazazi wote wawili wa mgombea urais wawe raia wa Kongo.

Mgombea mwengine ni Martin Fayulu, ambaye anaamini kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi wa 2018 na kwamba Tshisekedi aliingia madarakani kinyume na sheria.

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel wa mwaka 2018, Denis Mukwege, naye pia ameingia kwenye kinyang'anyiro hicho, jambo linalozidisha mkanganyiko kwa wapigakura wa upinzani.

Nafasi ya Mukwege

Mwanadiplomasia mmoja mjini Kinshasa aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Mukwege "ana uhalali wa kimaadili" wa kuwa rais wa Kongo, hasa kutokana na kazi yake ya kupambana na dhuluma za kingono mashariki mwa nchi yake.

Denis Mukwege, mgombea urais wa Kongo na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel.Picha: Giscard Kusema/Präsidentschaft der Demokratischen Republik Kongo

Hata hivyo, daktari huyo wa masuala ya wanawake hafahamiki sana nje ya ngome yake ya mashariki na hata baadhi ya maeneo yanamchukulia kuwa ni mgombea anayeungwa mkono na mataifa ya Magharibi, sifa isiyofaa kwa siasa za Kongo.    

Soma zaidi:  Mukwege akosoa matayarisho uchaguzi DRC
      
Akitangaza nia yake ya kuwania nafasi hiyo tarehe 2 Oktoba, Mukwege aliwaambia wafuasi wake kwamba "umoja wa makundi yote ni muhimu" kwenye kuibadilisha nchi yao.
  
Kwa mujibu wa Moleka, Mukwege yuko tayari kuungana na wagombea wengine kumsimamisha mtu mmoja kupambana na Tshisekedi, lakini haifahamiki kuhusiana na wanasiasa wengine wanaotaka wadhifa huo.

Baadhi ya wachambuzi wanasema huenda mgombea mmoja wa upinzani akapatikana mwishoni mwishoni kabisa mwa kampeni ili kuepuka hujuma za serikali dhidi yao. 

Wasiwasi wa upinzani

Wagombea wa upinzani wamekuwa wakilalamikia kile wanachokiita "kufinyika kwa demokrasia" kufuatia hujuma na mashambulizi kadhaa dhidi yao.

Upinzani nchini Kongo una wasiwasi wa ikiwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki.Picha: Nicolas Maeterlinck/Benoit Doppagne/Ute Grabowsky/picture alliance

Mwanasiasa wa upinzani kutokea chama cha Katumbi, Cherubin Okenda, aliuawa mjini Kinshasa mnamo mwezi Julai katika mazingira ya kutatanisha.

Soma zaidi: Upinzani Kongo wataka wachunguzi kutoka nje mauaji ya Okende

Vile vile, kuna mwandishi mmoja wa habari ambaye amefungwa jela kwa tuhuma za "kusambaza habari za uzushi" juu ya mauaji hayo.

Kongo, taifa kubwa zaidi na lenye migogoro mingi zaidi katikati ya Afrika, linaelekea kufanya uchaguzi mkuu wa wabunge, maseneta na rais mnamo tarehe 20 Disemba.

Orodha rasmi ya Tume ya Uchaguzi (CENI) inatarajiwa kuchapishwa tarehe 25 Oktoba, huku vyama vingi vya upinzani vikiamini kuwa uchaguzi huo utakuwa na wizi mkubwa wa kura.

Vyanzo: AFP, Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW