1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi kuapishwa kuwa rais wa Kongo

Josephat Charo
24 Januari 2019

Felix Tshisekedi anatarajiwa kuapishwa kuwa rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasai ya Congo leo (24.01.2019) katika hatua ya kwanza ya kihistoria tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

DR Kongo Politiker Felix Tshisekedi
Picha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Shughuli ya kuapishwa Tshisekedi zitafanyika katika ikulu ya rais mjini Kinshasa kuanzia saa sita kamili saa za Congo. Tshisekedi mwenye umri wa miaka 55, atachukua mikoba ya uongozi kutoka kwa rais Kabila, ambaye sasa akiwa na umri wa miaka 47, ameitawala Congo kwa miaka 18, baada ya kumrithi marehemu baba yake Laurent-Desire Kabila, aliyeuliwa mwaka 2001.

Katika hotuba ya mwisho kwa taifa hapo jana iliyooneshwa moja kwa moja katika televisheni ya taifa RTNC, rais Kabila amesema hataiendea kinyume katiba ya nchi hiyo.

"Kwa kuheshimu katiba nitakabidhi madaraka pasipo kuwa na majuto wala kutubu kwa sababu licha ya mapungufu yanayotokana na kazi zote za mkono wa binadamu, Congo imetoka mbali na imepiga hatua kubwa na leo iko katika msingi imara."

Katika hotuba hiyo ambayo ilikuwa ya kwanza tangu uchaguzi uliofanyika Desemba 30 mwaka uliopita, Rais Kabila pia ametoa mwito wa umoja wa kitaifa akitaka paundwe muungano wa vyama mbali mbali vya kisiasa, ambao utawakabili wale ambao wameungana na watakaojaribu kila mara kushirikiana kumiliki na kujinufaisha na raslimali za Congo.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya CongoPicha: Reuters/K. Katombe

"Muungeni mkono Tshisekedi"

Kabila alijitapa kwa kufanikisha mengi ikiwa ni pamoja na kuliunganisha taifa na kudhibiti mfumuko wa bei. Rais huyo akawa na ujumbe kwa wananchi wote wa Congo. "Nawasihi mumuunge mkono kwa wingi kama vile mlivyoniunga mkono mimi katika kipindi cha miaka 18 iliyopita. Nawatolea wito hususan vijana wetu, ambao ndio mustakabali wa taifa letu."

Licha ya ushindi wake kutiliwa shaka, Tshisekedi amepata uungwaji mkono muhimu kutoka kwa Marekani na nchi mbili jirani, Angola na Jamhuri ya Congo, huku idadi ya mataifa yanayoukubali ushindi wake ikiendelea kuongezeka. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Robert Palladino, alisema Marekani inaukubali na kuupongeza uamuzi wa mahakama ya katiba kumthibitisha Tshisekedi kama rais mpya wa Congo.

Rais wa Angola, Joao Lourenco amemtakia kila la kheri Tshisekedi katika utekelezaji wa majukumu ya kazi yake ngumu aliyopewa na wakongomani.

Mataifa mengine kadhaa ya Afrika yamempongeza Tshisekedi yakiwemo Afrika Kusini, Kenya, Tanzania, Burundi na Misri.

Mwandishi: Josephat Charo/dpae/afpe/ape

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW