1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi: Rwanda imepeleka raia wake maeneo ya M23

12 Desemba 2024

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, amesisitiza mbele ya wabunge kwamba raia wa Rwanda wamewekwa kwenye vijiji vya kimkakati katika jimbo la Kivu Kaskazini, vilivyotekwa na waasi wa M23.

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Picha: DW

Wakati wa hotuba yake mbele ya bunge, Rais Félix Tshisekedi alilaani mkakati unaodaiwa kuratibiwa na Rwanda wa kubadilisha uwiano wa idadi ya watu katika baadhi ya maeneo ya Kivu Kaskazini.

Alisisitiza kuhusu kutolewa kwa watu kwenye maeneo ya kimkakati na kisha kupandikizwa na raia wa Rwanda.

"Zaidi ya uhamisho mkubwa wa watu unaosababishwa na vita, kuna jambo la kutisha linaloendelea: upunguzaji wa watu kwenye maeneo ya kimkakati ukifuatiwa na kupandikizwa kwa watu wa kigeni walioletwa na Rwanda. Hali hii inazua changamoto kubwa kuhusu uhuru wa kitaifa na uwiano wa idadi ya watu, na inahitaji majibu ya haraka na ya pamoja." amesema kiongozi huyo.

Rais pia alikumbusha kwamba zaidi ya Wakongo milioni tano wamehamishwa kutokana na vita hivi, wakiacha nyumba zao ambazo sasa zinakaliwa na watu wageni.

Kundi la M23 halijakataa madai hayo na linadai kuwa watu hao ni Wakongo waliokuwa wakimbizi kwa zaidi ya miaka 30 katika nchi jirani za maziwa makuu.

Hali hii inaleta wasiwasi katika masuala ya uhuru wa kitaifa na kuzua migogoro ya ardhi katika eneo ambalo tayari limeharibiwa na vita.

Duru kadhaa zasema madai ya Tshisekedi yana ukweli 

Kwa mujibu wa chanzo cha ndani kilichoomba kutotajwa jina, jambo hili ni la kweli na linazua hofu kubwa kwa watu waliokimbilia Goma.

"Taarifa ni ya kweli. Hadi sasa hatujui kama ni serikali ya Rwanda inayowaleta au kama wanakuja wenyewe. Hofu ni kwamba, vita ikimalizika na sisi ambao tupo Goma tukihitaji kurudi, hakika kutakuwa na migogoro ya ardhi."

Waasi wa M23.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Vyanzo vya ndani katika maeneo yanayodhibitiwa na M23 vinaripoti kwamba waasi wamewatumia ujumbe wakimbizi, wakiwataka warudi vijijini kwao vinginevyo nyumba zao na mashamba yao yatapewa watu wengine.

Hata hivyo, M23 inadai kwamba watu waliowekwa katika maeneo hayo ni Wakongo waliokuwa wakirejea kutoka uhamishoni.

Lawrence Kanyuka, msemaji wa Muungano wa Mto Kongo unaojumuisha M23, amesema;

"Watu wanaozungumziwa ni raia wa Kongo waliokimbilia nchi mbalimbali za Ukanda wa Maziwa Makuu kwa zaidi ya miaka thelathini. Wenzetu, ambao baadhi ya watu wanataka kuwakosesha uraia, walikimbia mauaji na mauaji ya kimya yaliyofanywa dhidi yao mnamo 1994 na Interahamwe FDLR walipoingia DRC.”

Mgogoro kati ya Rwanda na DRC una mizizi katika historia ngumu ya uhamiaji, vita, na mapambano ya kugombea mamlaka. Swali la watu waliohamishwa na uwekaji wa watu katika maeneo ya kimkakati linaendelea kuwa suala nyeti, likichochea mvutano na wasiwasi kuhusu mustakabali wa eneo hilo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW