1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi: Rwanda iwekewe vikwazo kwa kuwaunga mkono M23

26 Septemba 2024

Rais Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix Tshisekedi ameitolea wito Jumuiya ya kimataifa kuiwekea Rwanda vikwazo kutokana na kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaoendesha vita mashariki mwa nchi hiyo.

Rais wa DRC Félix Tshisekedi akihutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Rais wa Kongo Félix Tshisekedi akihutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: Leonardo Munoz/AFP/Getty Images

Tshisekedi ameitoa kauli hiyo wakati mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini NewYork ukiingia siku yake ya tatu ambapo viongozi mbalimbali wataendelea kuhutubia juu ya changamoto zinazoikabili dunia ikiwa ni pamoja na vita na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

Tshisekedi ambaye ametaka kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda katika ardhi ya Kongo, amesema uchokozi wa jirani yake unakiuka uhuru wa taifa hilo huku akisisitiza kuwa kuibuka tena kwa kundi la M23 kumesababisha mgogoro wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa na kwamba  Rwanda  inawajibika katika kuvuruga utulivu wa nchi hiyo.

Kwa miongo kadhaa sasa, eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri mkubwa wa madini limekuwa likishuhudia ghasia za makundi yenye silaha ambazo zimesababisha maafa makubwa.

Soma pia: UN: Wataalamu wasema wanajeshi kati ya 3,000 na 4,000 wa Rwanda walipelekwa nchini Kongo

Viongozi wengine wa Afrika waliyohutubia jana Jumatano  ni pamoja na yule wa Ghana, Namibia, visiwa vya Ushelisheli, Libya na Madagascar. Siku ya Alhamisi, viongozi wengine wa mataifa ya Afrika watakaopanda jukwaani ni marais wa Malawi, Cameroon, Kenya,  Burundi, Gabon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gambia, Lesotho, visiwa vya Comoros, Sudan na Sudan Kusini.

Macron: Diplomasia ipewe kipaumbele, mzozo wa Mashariki ya Kati 

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha: Dominique Jacovides/abaca/picture alliance

Miongoni mwa marais wengine waliohutubia usiku wa jana ni pamoja na yule wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye aliizungumzia mizozo ya  Mashariki ya Kati  pamoja na ule wa Ukraine. Kuhusu mzozo unaoendelea kutokota kati ya Israel na kundi la Hezbollah la Lebanon, Macron amesema diplomasia ndiyo inayotakiwa kupewa kipaumbele katika kuutatua mzozo huo.

Rais huyo wa Ufaransa amekuwa kiongozi pekee wa nchi za Magharibi aliyefanya mazungumzo na rais wa Iran Massoud Pezeshkian na kumtaka kutumia ushawishi wake ili kuishinikiza Hezbollah kutouchochea mzozo huo.

Mzozo kati ya Israel na Hezbollah wapamba moto

01:29

This browser does not support the video element.

Ama kuhusu vita vya Gaza, Macron amesema Israel ina haki ya kujilinda lakini mzozo huo umefikia pabaya huku akihimiza kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha vita, huku akitoa wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanyiwa mageuzi kuhusu mfumo wa matumizi ya kura ya turufu hasa yanapohusishwa matukio ya mauaji ya watu wengi.

Wakati wa hotuba yake, Macron ameiahidi Ukraine kuwa wataendelea kuipatia silaha inazozihitaji ili kujilinda na uvamizi wa Urusi na kusema nchi yake inawaunga mkono raia wa Ukraine kwa ujasiri wao wa kukabiliana na Urusi.

Zelensky aishutumu Urusi huku akikosolewa na Trump

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akihutubia Mkutano wa Baraza Kuu la UNPicha: Bryan R. Smith/AFP

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ni miongoni mwa waliohutubia jana jioni na hotuba yake ilijikita katika kutafuta uungwaji mkono zaidi wa viongozi wa dunia pamoja na kuishutumu Urusi kuwa inapanga mashambulizi dhidi ya vinu vyake vya nyuklia ambayo yanaweza kusababisha maafa makubwa. Zelensky amesema Moscow imekuwa ikifanya ukaguzi wa vinu vya nyuklia vya Ukraine kwa kutumia satelaiti.

Katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Zelensky alizinyooshea kidole China na Brazil huku akitilia mashaka maslahi ya nchi hizo ambazo zimekuwa zikiishinikiza Ukraine kufanya mazungumzo na Urusi. Zelensky ameziambia China na Brazil kuwa hazitojiimarisha kwa kuikandamiza Ukraine na kwamba dunia tayari imepitia vita vya kikoloni na njama za madola makubwa kwa gharama ya mataifa madogo.

Soma pia: Zelensky: Urusi inapanga kushambulia mitambo yetu ya nyuklia

Mara baada ya hotuba hiyo, mgombea urais wa Marekani kupitia tiketi ya chama cha Republican Donald Trump alimwita Zelensky "mfanyabiashara mkuu zaidi Duniani," na kusema kuwa kila wakati Zelensky anapokwenda Marekani, huondoka na mabilioni ya dola. Trump alisema vita hivyo havitokwisha isipokuwa atakapochaguliwa tena kuwa rais. Marekani imetoa takriban dola bilioni 175 kwa msaada wa kijeshi na kiuchumi kwa Ukraine tangu Urusi ilipovamia mnamo Februari mwaka 2022.

Mshirika mwingine wa Ukraine ambaye ni Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, ameliambia hapo jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Putin amekuwa akiwatuma raia wake kwenye kifo mithili ya kuwabwaga kwenye mashine ya kusagia nyama huku akihoji ni jinsi gani Urusi inaweza kuonyesha uso wake katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

(Vyanzo: AP, DPAE, Reuters, AFP)