Tsipras kukutana na Putin
8 Aprili 2015Ziara hii ya siku mbili inakuja wakati ambapo Tsipras anapambana kupata sehemu iliyobakia ya kile kiitwacho "fedha za uokozi" kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Umoja wa Ulaya.
Hadi sasa, Ugiriki haijafikia makubaliano na wakopeshaji wake hao juu ya kulipa sehemu ya deni lake la awali, kabla ya kupewa sehemu hiyo iliyobakia.
Serikali ya Ugiriki imesema inatazamia mkutano wa manaibu mawaziri wa fedha wa sarafu ya euro wanaokutana kuandaa kikao cha mawaziri wao utafungua njia ya kuutatua mkwamo uliopo.
Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kwenye makao makuu ya Umoja huo, Brussels, wameonya kwamba hatua yoyote ya Ugiriki kuelekea Urusi inamaanisha taifa hilo la Ulaya linatafuta uungwaji mkono kifedha na kisiasa nje ya Umoja huo, kauli ambayo imekanushwa na serikali ya Ugiriki hivi leo, ikisema nchi hiyo haijaomba msaada wowote wa kifedha kutoka Urusi na kwamba imekusudia kusaka suluhisho la matatizo yake ndani ya Umoja wa Ulaya.
Afisa mmoja wa serikali ya Ugiriki alisema Tsipras na Putin watajadiliana tu ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji baina ya mataifa yao, ukiwemo usafirishaji wa bidhaa na kwamba hayo yatafanyika kwa misingi iliyowekwa na Umoja wa Ulaya.
"Ugiriki inajuwa jambo la kufanya ndani ya mfumo wa Umoja wa Ulaya, lakini kila nchi ina haki na mamlaka ya kutafuta na kuimarisha mahusiano yake na nchi nyengine," alisema afisa huyo.
Bunge la Ulaya laonya
Kabla ya ziara hii kuanza, Spika wa Bunge la Ulaya, Mjerumani Martin Schulz, alimuonya Tsipras juu kuvuuka mstari wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, ambavyo Umoja huo umeviweka kwa kuituhumu Urusi kuhusika na mzozo wa Ukraine. Tsipras, ambaye ni mkomunisti wa zamani aliyeingia madarakani mwezi Januari mwaka huu, hafanyi siri katika kusaka kwake mafungamano na Urusi.
Waziri wa kilimo wa Urusi alisema hapo jana kwamba nchi yake inaweza kufikiria kuziondoa Ugiriki, Hungary na Cyprus kwenye orodha ya nchi za Magharibi zilizouiwa kuingiza chakula nchini Urusi, hatua iliyochukuliwa kujibu vikwazo ambavyo viliwekwa kujibu hatua ya mataifa ya Magharibi dhidi ya Urusi.
Gazeti la kila siku la masuala ya biashara ya Urusi, Kommersant, hapo jana lilikinukuu chanzo kimoja serikalini, kikisema kuwa Urusi inaweza pia kuipa Ugiriki punguzo la bei ya gesi na pia mikopo mipya.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga