1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuchel ataka kukamilisha kileleni mwa Bundesliga

Josephat Charo
10 Agosti 2023

Katika msimu mpya wa Bundesliga kocha klabu ya Bayerfn Munich Thomas Tuchel amesema anataka kukamilisha kileleni wa jedwali. Nia yake pia ni kushinda kombe la shirikisho la Ujerumani na kombe la mabigwa wa Ulaya.

Fussball, Herren, Saison 2022/2023, FC Bayern München, Pressekonferenz, Thomas Tuchel, Allianz Arena
Picha: Ulrich Wagner/picture alliance

Kocha wa Bayern Munich Thomas Tuchel anataka kukamilisha kileleni katika mashindano mengi kadri inavyowezekana msimu ujao kwa kuwa bado pana fursa ya kujiimarisha baada ya msimu uliopita.

Bayern walilazimika kupambana sana katika ligi kuu ya Bundesliga kuwapokonya ubingwa Borussia Dortmund mechi ya mwisho ya msimu uliopita, lakini kutolewa mapema nje ya kombe la shirikisho la Ujerumani DFB Pokal na kombe la mabingwa wa Ulaya yalikuwa matokeo yaliyo chini ya matamanio yao.

Tuchel, aliyechukua mikoba kutoka kwa kocha wa zamani Julian Nagelsmann mwishoni mwa mwezi Machi, ameliambia jarida la klabu ya Bayern katika mahojiano yaliyochapishwa kwa sehemu kwenye tovuti yao Jumatano (09.08.2023) kwamba ameipenda hulka ya Bayern kushinda tangu siku za utotoni na analenga kuwa kileleni katika msimu wake wa kwanza kamili.

"Tunataka tuwe mabingwa, hatimaye tufanikiwe kucheza fainali ya kombe la shirikisho mjini Berlin kwa mara nyingine tena, na katika ligi ya mabingwa, FC Bayern wakati wote ni miongoni mwa timu kubwa zinazopambana kushinda taji," alisema.

Wachezaji wa Bayern baada ya ya mechi yao na Hertha Berlin 30.04.2023Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

"Katika yote haya, tunataka kuwafurahisha mashabiki. Kulinganisha na msimu uliopita, kuna fursa ya kufanya vyema zaidi, sote tunalifahamu hilo. Hatukutimiza matarajio wakati huo."

Soma pia: Bayern kumnasa Kane hatimaye?

Tuchel alitaja utambulisho wa wachezaji na klabu hiyo kama rasilimali kubwa kuelekea mafanikio kwa kuwa unavutia heshima ya hali juu kabisa nje ya nchi na pia timu inaogopwa.

"Huu ndio utambulisho hapa: kushinda, licha ya vizuizi vyote, hata kama huchezi vizuri mara nyingine. Kadri nilivyokua, niligundua ni jinsi gani kila kitu kinategemea fikra, ukakamavu, ari, kujiamini mwenyewe kikamilifu. Unaweza kuilazimisha bahati. Na halafu bahati maarufu inayohusishwa mara kwa mara na Bayern inabadilika na kugeuka kuwa ubora.

Mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich wanaanza msimu mpya Jumamosi katika pambano kali la kombe la Super Cup dhidi ya washindi wa kombe la shirikisho RB Leipzig. Wataanza Bundesliga siku sita baadaye ugenini na Werder Bremen.

(dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW