1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuhuma za wizi wa kura zazuwa mashaka uchaguzi Kenya

13 Agosti 2022

Kwa mara ya kwanza tangu utangazaji matokeo uanze, kumetolewa madai yasiyothibitishwa ya wizi wa kura kutoka kwa chama tawala nchini Kenya, Jubilee, ambacho kinamuunga mkono mgombea urais wa upinzani, Raila Odinga.

Kenia nach den Wahlen 2022
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee chake Rais Uhuru Kenyatta, ambacho kinamuunga mkono mgombea urais wa muungano wa Azimio, Raila Odinga, ametoa tamko ambalo linatuhumu kuwepo kwa kile alichokiita "wizi mkubwa wa kura", akidai kwamba "mchakato mzima wa uchaguzi umeingiliwa". Hii ni baada ya chama cha hasimu wa Raila, Naibu Rais William Ruto, kuonesha mafanikio makubwa kabisa kwenye maeneo ambayo kawaida yanachukuliwa kumuunga mkono Kenyatta.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, pamoja na mengine, tamko hilo linatuhumu kutishwa kwa wapigakura, rushwa, kuwepo kwa mabango ya kampeni kwenye vituo vya kupigia kura, kutendewa vibaya kwa mawakala wa vyama vya siasa na matumizi yasiyo sahihi ya vifaa vya uchaguzi. 

Hata hivyo, Reuters haikuwapata maafisa wa chama hicho kuzungumzia madai hayo, ambayo yanakwenda kinyume sana na matamshi ya waangalizi wa kimataifa ambao wameusifia mchakato mzima wa uchaguzi wa uwazi, huru na wa haki.

Chaguzi zilizopita nchini Kenya zilikuwa zikiamuliwa na kile kinachoitwa "hisabati za kikabila", lakini kwenye uchaguzi wa mara hii, Ruto anatajwa kujenga kampeni yake juu ya masuala ya uchumi, akijieleza kama "mchakarikaji" wa mitaani dhidi ya wale anaowaita wanasiasa wa himaya za kifalme. Odinga na Kenyatta ni watoto wa makamu wa kwanza wa rais na rais wa Kenya.  

Kusuwasuwa kwa matangazo ya matokeo kwazusha wasiwasi

William Ruto (kushoto) na Raila Odinga wakipiga kura zao siku ya Jumanne (Agosti 9).Picha: AFP

Kwa upande mwengine, kuendelea kuchelewa kutangazwa kwa matokeo rasmi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kunazusha wasiwasi miongoni mwa wananchi.

Tume hiyo, ambacho ndicho chombo pekee chenye mamlaka ya kisheria kumtangaza mshindi, awali iliweka mtandaoni picha za fomu za matokeo kutoka zaidi ya vituo 46,000 vya uchaguzi, lakini haikuwa imezifanyia majumuisho. Badala yake, vyombo vya habari vilitumia timu zake kuzipakuwa fomu hizo na kuingiza matokeo kwenye kanzidata. 

Zaidi ya asilimia 99.7 ya matokeo kutoka vituoni tayari yapo kwenye mtandao, lakini maelfu kwa maelfu hayajajumuishwa na vyombo vya habari. Kushuka huko kwa kasi ya ujumuishaji matokeo kulianza wakati takribani asilimia 80 ya kura zimekamilika kuhesabiwa.

Hadi vyombo vya habari vilipositisha kutangaza majumuisho yao asubuhi ya jana Ijumaa, matokeo yalikuwa yakionesha Ruto na Odinga wakichuwana vikali huku pakiwa hakuna hata mmoja aliyempita mwenzake kwa zaidi ya asilimia moja. Ikiwa hakutakuwa na mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50, mahasimu hao wawili watapaswa kurudi kwenye duru ya pili ya uchaguzi.

Asubuhi ya jana, IEBC, ambayo ina siku saba tu za kukamilisha kutangaza matokeo tangu kumalizika kwa uchaguzi, ilichapisha matokeo rasmi ya urais kwenye ubao wake katika kituo kikuu cha majumuisho, lakini ikiwa imekamilisha asilimia 1.5 tu ya kura zote. 

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, amewalaumu mawakala wa vyama vya siasa kwa kasi ndogo ya uhisabuji wa kura, akisema lazima zoezi hilo likamilike haraka iwezekanavyo.