1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Tume Senegal yapendekeza uchaguzi Juni 2

28 Februari 2024

Tume ya taifa ya majadiliano nchini Senegal imependekeza uchaguzi wa rais uliochelweshwa nchini humo ufanyike Juni na Rais Macky Sall kusalia madarakani hadi mrithi wake atakapoapishwa.

Hotuba ya TV| Rais wa Senegal Macky Sall
Tume ya majadiliano yapendekeza Rais Macky Sall asalie madarakani hadi mrithi wake atakapoapishwa.Picha: RTS/Reuters

Mapendekezo hayo yanafuatia siku mbili za mazungumzo yaliyoandaliwa na Sall kwa lengo la kupunguza mvutano na kukubaliana juu ya njia ya kuondoka kwenye mzozo wa kisiasa wa takriban mwezi mzima.

Jaribio lake na la bunge lililoshindwa kuahirisha uchaguzi wa Februari 25 kwa miezi kumi limezusha machafuko na kauli za kutahadharisha juu ya kuporomoka  kwa demokrasia.

Mazungumzo hayo yaliofanyika katika mji mkuu wa Dakar yalisusiwa na wanasiasa wengi wa upinzani ambao baadhi yao wanataka uchaguzi ufanyike kabla ya muda wa kukaa madarakani rais  Macky Sall kumalizika tarehe 2 Aprili.

Soma pia:Sall atangaza kuondoka madarakani Aprili 2 

Haikuweza kufahamika mara moja jinsi watakavyojibu tarehe iliyopendekezwa ya Juni 2. Hata hivyo, mmoja wa washiriki wa mazungumzo hayo Amar Thioune, alisema waliokuwepo wanawakilisha sehemu kubwa zaidi ya jamii ya Senegal.

Uamuzi wa Rais Sall kuahirisha tarehe ya uchaguzi ulisababisha hasira na maandamano kote nchini SenegalPicha: John Wessels/AFP

"Ukweli ni kwamba unapokuwa na vyama vikuu, vyama vya kiraia, viongozi wa kidini na kimila, ambao wote walikuwepo, walikuwa na ujumbe mmoja," alisema Thioune.

Soma pia: Rais Macky Sall apendekeza mswada wa msamaha Senegal

"Nadhani kwamba, kwa maslahi ya amani na utulivu katika nchi yetu, hii ni muhimu kwa hali yoyote. Sitawasemea wagombea waliokataa kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa, wanapaswa kukubali, hasa kwa vile haki zao za msingi zimeheshimiwa."

Taifa hilo lenye utulivu la Afrika Magharibi linapambana na mzozo wake mbaya zaidi wa kisiasa kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa baada ya Sall kuahirisha uchaguzi wa Februari 25 katika muda wa mwisho.

Baraza la Katiba lilibatilisha ucheleweshaji huo na siku ya Jumatatu Rais Sall alizindua mazungumzo ya siku mbili kuweka tarehe mpya, ambayo hata hivyo yaliyosusiwa na wahusika wakuu wa kisiasa na kijamii.

Mahitimisho ya kamati za majadiliano

Kamati mbili ziliundwa kujadili tarehe ya uchaguzi na mpangilio wa kipindi cha baada ya Aprili 2. Kamati ya kwanza ilifikia hitimisho la karibu kauli moja kwamba kura haingeweza kufanyika kabla ya Aprili 2. Kamati ya pili ilifikia makubaliano mapana ya kutaka Rais Sall abakie madarakani hadi mrithi wake atakapoapishwa.

Mabaliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama yamesababisha vifo vya watu wanne.Picha: Seyllou/AFP

Kamati hizo mbili zilipaswa kuwasilisha mapendekezo yao ya mwisho kwa rais jana jioni, lakini hakukuwa na dalili yoyote kuhusu lini Sall angefanya uamuzi. Wiki iliyopita, alisema atapanga tarehe mara moja ikiwa kutakuwa na makubaliano.

Soma pia:Wagombea 15 Senegal wataka kura kabla ya rais kuondoka 

Uamuzi wa Februari 3 wa kuahirisha uchaguzi wa rais uliitumbukiza Senegal katika machafuko, na watu wanne waliuawa katika makabiliano na vikosi vya usalama.

Sall, aliye madarakani tangu mwaka wa 2012, alisema alisitisha upigaji kura kufuatia mizozo juu ya kufutwa kwa baadhi ya wagombea na hofu ya kurejea kwenye machafuko kama mwaka 2021 na 2023. Lakini upinzani uliitaja hatua hiyo kuwa mapinduzi ya kikatiba.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW