Tume ya Haki za Binaadamu yaanza kazi DRC
22 Februari 2023Timu hiyo iliyoteuliwa kupitia agizo la Rais wa Kongo Felix Tshisekedi la Januari 31 inawajumuisha wajumbe wanne wanaounda ofisi yake wameanza rasmi kazi wakichukua nafasi ya timu ya zamani ambayo muda wake ulikuwa umekwisha, lakini wakaendelea kubaki ofisini kinyume na sheria.
Timu hiyo itashiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ukiukaji wa haki za kibinadamu, hasa mashariki mwa Kongo ambako raia wanakabiliwa na mashambulizi ya makundi ya waasi, likiwemo kundi la M23 linaloaminika kuungwa mkono na Rwanda.
Tume hiyo itazingatia diplomasia hai
Paul Nsapu, mwenyekiti mpya wa tume ya CNDH anasema hatua zao za msingi zitakuwa diplomasia hai, hasa hali ya uvamizi na mashambulizi mashariki mwa Kongo kuhusiana na masaibu, mateso ambayo wakaazi wanakumbana nayo.
''Katika mashambulizi hayo kuna ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Hicho ni kipaumbele chetu cha kwanza. Pia tutazipeleka sauti ya watu wa Kongo duniani kote," alifafanua Nsapu.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu, Brandt Kehris, amesema hali ya haki za binadamu mashariki mwa DRC inaendelea kutia wasiwasi.
Kehris ambaye amemaliza hivi karibuni ziara katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini amesisitiza kwamba kuna udharura ili kukomesha ghasia upande huo wa Kongo.
Kehris: Ukiukaji wa haki za binadamu ukomeshwe
"Kwa kweli kunahitajika uharaka kutokana na hali hii ya ukiukaji wa haki za binaadamu ambao lazima ukomeshwe. Pia mahitaji yote yanayotokana na hali hii ya usalama, ikiwa ni pamoja na watu wote waliokimbia huko. Changamoto zinazowakabili washiriki wote wakiwemo viongozi wa nchi wenyewe," alibainisha Kehris.
Kwa miaka kadhaa sasa wakaazi wa mikoa ya mashariki mwa Kongo wamekuwa wakikabiliwa na vita pamoja na ghasia nyingine zinazoendelea ambazo zimewalazimu maelfu yao kuvikimbia vijiji vyao.
Tume hii ya haki za binaadamu ya taifa, hata hivyo, haina nguvu za kuzuwia madhila haya, zaidi ya kukusanya ushahidi na ripoti kwa ajili ya vyombo vingine vyenye mamlaka kuchukuwa hatua.
(DW)