Tume ya jeshi la majini kutumwa pwani ya Libya
27 Aprili 2016Wakati wa ziara yake barani Ulaya rais Obama alikutana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa Ufaransa Francoise Hollande, waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron na waziri mkuu wa Italia, Matteo Renzi, mjini Hannover (25.04.2016) kujadiliana kuhusu hatua moja madhubuti ambayo huenda ikasaidia kuondosha vitisho vya kimkakati vinavyolikabili bara la Ulaya: kuunda tume ya pamoja katika pwani ya Libya itakayokuwa na umuhimu mkubwa kimkakati na pengine kwenda mbali zaidi katika kuyashughulikia malalamiko ya rais Obama kuhusu viongozi wanaotegemea usalama kutoka Marekani na wanaoiburuza Marekani kujiingiza katika miradi ya gharama kubwa ambayo hata huwa haina umuhimu wowote kwa usalama wa taifa.
Msingi halisi wa wasiwasi wa Obama kuhusu Ulaya unaweza kushuhudiwa katika mzozo wa wakimbizi ambao umekuwa wimbi zito linalouhatarisha mradi wa Ulaya yenye umoja. Wimbi la wahamiaji kutoka maeneo ya kusini na mashariki mwa Ulaya limesababisha janga kubwa la kibinaadamu, kuua idadi isiyojulikana ya watu, kuwapa changamoto viongozi kuhusiana na misimamo yao kimaadili na kuyaacha mashirika ya misaada yakijizatiti kuwasaidia wahamiaji hao.
Pia imeongeza kitisho cha kundi la Dola la Kiislamu kulitumia wimbi la wakimbizi kama mbinu ya kuwaingiza wapiganaji wake kupanga mashambulizi katika ardhi ya Ulaya kama yale yaliyofanywa mjini Paris nchini Ufaransa mwaka uliopita na mjini Brussels, Ubelgiji mwaka huu. Yote haya yamechochea makundi ya kizalendo ya Ulaya na mavuguvugu ya mrengo wa kulia ambayo mara kwa mara hupinga kuwajumuisha wageni katika jamii na kupanda mbegu ya chuki na kuiyumbisha jamii. Madai kwamba Urusi imehusika katika kuyadhamini makundi ya aina hii yameitia wasiwasi serikali ya Marekani kwa muda mrefu.
Uzoefu katika bahari ya Aegean kutumika
Obama na washirika wake wa Ulaya tayari wamekubaliana kuratibu kikosi cha jeshi la majini katika bahari ya Aegean kuwafautilia wafanyabiashara haramu ya kusafirisha binaadamu, kwa lengo la kuzuia boti za wahamiaji zisifike katika visiwa vya Ugiriki kutokea nchini Uturuki.
Sasa viongozi wa Ulaya na Marekani wanatafakari kwa pamoja kuona kama kitu kama hicho kinaweza kufaulu katika pwani ya Libya ambayo ni kubwa zaidi na yenye hatari kubwa.
Kwa mujibu wa ikulu ya Marekani, washirika huenda wakatumia uzoefu uliopatikana katika bahari ya Aegean kutafuta njia ambazo wanaweza kushirikiana kulikabili tatizo la wakimbizi kukimbilia Ulaya kupitia bahari ya Mediterania kwa ufasaha na kwa kuheshimu utu wa kila binaadamu. Inakadiriwa watu 350,000 wamefanya safari kutoka Libya kupitia baharini kwenda Italia tangu mwanzoni mwa mwaka 2014. Katika kipindi hicho kundi la dola la kiislamu limekuwa likijiimarisha nchini Libya.
Maswali yangalipo
Maswali mengi yamejitokeza kuhusu mpango huo yakiwemo: Je, tume hiyo itakuwa chini ya jumuiya ya kujihami ya NATO au Umoja wa Ulaya? Je ni kwa kiwango gani itategemea ufuatiliaji, taarifa za kijasusi na nyenzo nyingine za Marekani, na je ni kipi kitakachofanywa kwa wahamiaji watakaokamatwa wakiwa njiani kuelekea Ulaya? Mataifa ya kigeni kwa hivyo yatatakiwa kuwa na uangalifu mkubwa katika kuiunda tume hiyo.
Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, inayogombania madaraka na makundi ya waasi na serikali hasimu, haitaki kusikia mijadala mingi kuhusu majeshi ya mataifa ya kigeni kuingilia kati nchini humo, hatua ambayo huenda ikavuruga uhalali wake. Matokeo yake ni kwamba mjadala wa nchi za Magharibi kuhusu kupeleka kikosi cha ardhini Libya kuwafurusha wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu katika mji wa Sirte, umezimwa.
Tume ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji katika pwani ya Libya haitarajiwi kuimarisha matumizi ya kijeshi ya Ulaya, kuainisha mchakato wa kupitisha maamuzi katika Umoja wa Ulaya au kukomesha uagizaji mara mbili wa vifaa vya kijeshi unaoababisha matumizi mabaya ya fedha. Lakini hata hivyo itapunguza mzozo ambao umemtia tumbo joto rais Obama kiasi cha kujiingiza katika siasa za Ulaya.
Mwandishi: Josephat Charo/afpe
Mhariri:Yusuf Saumu