1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi DRC yaongeza muda wa kuandikisha wapigakura

23 Januari 2023

Tume Huru ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, CENI imeongeza siku 25 za muda wa kuandikisha wapiga kura.

Wahlen in Kongo 28.11.2011
Picha: picture-alliance/dpa

Muda huo umeongezwa katika eneo la kwanza linalohusika na zoezi hilo nchini Kongo. Shughuli hiyo iliyoanza Desemba 24, 202 katika mikoa ya magharibi mwa Kongo ilikuwa imepangwa kukamilika siku ya Jumatatu Januari 23. Hata hivyo, hadi sasa CENI imeorodhesha chini ya nusu ya idadi ya wapiga kurawanaotarajiwa katika uchaguzi wa Desemba 2023. 

Kati ya watu zaidi ya milioni 18 wanaotarajiwa kujiandikisha katika mikoa hiyo ikiwemo na mji mku, Kinshasa ni watu milioni 7.9 tu, yaani asilimia 37.9, ndiyo tayari wamepokea vitambulisho vyao vya kupigia kura.

Muda waongezwa kutokana na kasoro zilizojitokeza

Hayo ni kutokana na kasoro zilizoonekana katika baadhi ya vituo vya usajili. Na sasa Tume Huru ya Uchaguzi, CENI imeamua kuongeza siku 25 za ziada ili kuwaruhusu Wakongo wote wanaostahili kupiga kura wapate vitambulisho vyao vipya na hivyo kupiga kura.

Msemaji wa tume ya uchaguzi, Patricia Nseya amesema CENI ilikutana ili kutathmini na kuchambua hali hiyo. ''Kutokana na uchanganuzi huo tumetambua kwamba idadi kubwa ya watu bado hawajajiandikisha na hivyo, CENI imeamua kutoa muda wa siku 25 za ziada kwa shughuli ya usajili wa wapiga kura katika eneo la kwanza la operesheni hiyo," alisema Nseya.

Mpiga kura akionesha karatasi za wapiga kura zilizopatikana kwenye baadhi ya maeneo Picha: AP

Miongoni mwa kasoro zilizobainishwa hivi karibuni na mashirika ya kiraia, ni pamoja na kuharibika vifaa vya usajili, watumishi wa CENI kuomba rushwa na kutokuwepo kwa baadhi ya vituo ingawa vimeandikwa kwenye ramani. Mambo ambayo CENI iliahidi kuyaboresha.

Lakini upande wa mashirika ya kiraia bado yana hofu kwani siku 25 za ziada hazijatosha. Dieudonné Mushagalusa ambaye ni mratibu wa wataalamu wa mashirika ya kiraia nchini Kongo, ameiambia DW kwamba Wakongo hawana imani kuwa watasajiliwa kwa muda na ipasavyo.  

Wakongomani wanaona mambo hayaendi sawa

"Mambo yanazorota kabisa. Mwezi mzima hawakukaribia nusu ya milioni 18 ambayo wanatayarisha. Wangali chini ya milioni kumi ya watu. Siku ambazo wameongeza hazifikii muda ambao wamekwishatumia," alifafanua Mushagalusa.

Kwa mujibu wa Mushagalusa, inaonekana vile vile hawatamaliza, kwani hawakujitayarisha, hawakuweza kurekebisha mambo yaliyopita na wana hofu kwamba hilo litakuwa jambo baya kushinda mengine yote.

Uchaguzi huo mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 20, 2023 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo utajumuisha uchaguzi wa rais, wa wabunge wa kitaifa na wa majimbo, pamoja na uchaguzi wa manispaa.