Tume ya uchaguzi Pakistan kuamua kesho kuhusu uchaguzi
31 Desemba 2007Tume ya uchaguzi nchini Pakistan inasema uamuzi kuhusu uchaguzi uliopangwa kuanyika tarehe 8 mwezi ujao wa Januari, utatangazwa hapo kesho.
Afisa wa serikali wa ngazi ya juu amesema uchaguzi huo huenda uahirishwe kwa majuma kadhaa. Afisa huyo wa serikali amesema uchaguzi huo utaahirishwa kwa sababu ya machafuko yanayoendelea nchini Pakistan ambayo yamewaathiri maafisa wa uchaguzi na shughuli za maandalizi ya uchaguzi huo.
Serikali inasema uratibu umetatizwa katika mkoa wa Sindh, nyumbani mwa familia ya Benazir Bhutto na kwamba uchapishaji wa makaratasi ya kupigia kura katika mji mkubwa wa Pakistan, Karachi umechelewa mno. Ofisi zaidi ya 40 za tume ya uchaguzi na ofisi za utawala zimeharibiwa katika mkoa wa Sindh.
Chama cha Pakistan People´s Party, PPP, cha marehemu Benazir Bhutto, kimepinga vikali njama ya kuuchelewesha uchaguzi huo, kikisema kiko tayari.
Msemaji wa chama hicho, Mahmoud Qureshi, amesema iwapo serikali itauchelewesha uchaguzi, watafanya kikao cha kamati kuu ya chama kujadili hatua watakayochukua.