1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi ya Libya yakataa kumuidhinisha al-Islam

25 Novemba 2021

Tume ya uchaguzi nchini Libya imekataa kumuidhinisha Seif al-Islam Gadhafi, mwanawe Moamer Gadhafi, kuwania Urais katika uchaguzi mkuu ujao wa Disemba 24.

Libyen | Protest gegen Präsidentschftskandidat Saif al-Islam al-Gaddafi
Picha: Hamza Alahmar/AA/picture alliance

Katika taarifa, tume hiyo ya uchaguzi ya HNEC imesema imekataa kumuidhinisha al-Islam anayesakwa na mahakama ya kimataifa ya jinai kwa tuhuma za uhalifu wa kivita. al-Islam alikuwa miongoni mwa wagombea wengine 25 ambao majina yao pia yalikataliwa.

Tume hiyo imesema imechukua uamuzi huo kwa misingi ya kisheria pamoja na kuzingatia taarifa kutoka kwa ofisi ya mwendesha mashtaka, mkuu wa polisi na idara ya kushughulikia hati za usafiri na uraia.

Tume hiyo imesema,"Majina yaliyotajwa yameondolewa kwenye orodha ya awali ya wagombea kwa kuwa hayakidhi matakwa na pia wagombea wamekosa kuwasilisha nyaraka zote muhimu."

Soma pia: Wahamiaji zaidi ya 5,000 wakamatwa Libya

Ama kuhusu Seif al-Islam, tume hiyo imenukuu kifungu cha sheria ya uchaguzi kinachosema, mgombea hafai kuwa na rekodi yoyote ya uhalifu. al-Islam hata hivyo anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Wagombea wengine wakiwemo mbabe wa kivita Khalifa Haftar, kaimu Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Fathi Bashagha wameidhinishwa kuwania Urais.

Libya inatarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu Disemba 24 

Saif al-Islam al-Gaddafi akijisajili kama mgombea wa UraisPicha: Khaled Al-Zaidy/REUTERS

Uchaguzi wa Disemba 24 unatokea katika wakati ambapo Libya inajaribu kufungua ukurusa mpya kufuatia vita vya muongo mmoja, vilivyolitikisa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta tangu kufanyika maandamano ya kushinikiza mageuzi yaliyosababisha kuuawa na kuondolewa madarakani kiongozi wa nchi hiyo kanali Moammer Gadhafi mnamo mwaka 2011.

Katika tangazo lililowashangaza wengi, Seif al-islam, ambaye alikuwa hajulikani aliko kwa miezi kadhaa, alikuwa wa kwanza kujitosa kwenye kinyang'anyiro cha Urais. al-Islam mwenye umri wa miaka 49, alihukumiwa kifo na mahakama ya mjini Tripoli kwa uhalifu uliofanywa wakati wa uasi uliompindua madarakani babake.

Soma pia: Muda wa kuondoka vikosi vya kigeni nchini Libya wamalizika

Hata hivyo, baadaye alisamehewa na utawala hasimu upande wa mashariki mwa Libya. Mnamo mwezi Julai, aliliambia gazeti la The New York Times, kwamba ananuia kujitosa kwenye ulingo wa siasa. Seif, alisema nia yake kuu ni kurudisha umoja wa Libya baada ya muongo mmoja wa machafuko.

"Naomba Mwenyezi Mungu alete haki baina ya watu wetu na tuchague watu waaminifu. Mungu ndiye anayeamua hata kama makafiri watachukia."

Tume ya uchaguzi ya Libya imetoa orodha ya wagombea 98 wa Urais wakiwemo wanawake wawili. Orodha ya mwisho ya wagombea wote watakaodhinishwa rasmi itachapishwa mapema mwezi ujao wa Disemba mara tu baada ya zoezi la kuwakagua kukamilika.