Tume ya uchaguzi ya Tanzania yataja baadhi ya wagombea urais
25 Agosti 2020Rais John Magufuli anakuwa mgombea wa kwanza kuwasili katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi mjini Dodoma akiambatana na mgombea mwenza ambae pia ni makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakiwa na dhima moja kurejesha fomu za kuwania nafasi ya urais walizochukua takriban wiki mbili zilizopita, ilii kuwania kipindi kingine cha miaka mitano kwa mujibu wa katiba ya taifa hili la Afrika Mashariki.
Wakikabidhi fomu hizo kwa NEC wamesema, wamekamilisha vigezo vyote vilivyotakiwa kwa mujibu wa sheria ikiwemo, idadi ya wadhamini kutoka mikoa 10 isipokuwa wameongeza mikoa mitano kama ziada hatua ambayo inaongeza idadi ya wadhamni kutoka ile 2,000 wanaohitajika kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.
Mkurugenzi wa NEC amesema uhakiki wao umethibitishwa vyema
Akiwasilisha kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi fomu hizo mkurugenzi wa NEC Dokta Charles Mahera amesema, wasimamizi wa uchaguzi wamethibitisha majina ya wadhamini ambao ni wapiga kura katika maeneo ambayo wagombea walifika kwa ajili ya kuomba udhamini.
Kando na mgombea wa chama tawala Dokta John Magufuli kufuzu kuteuliwa na tume ya uchaguzi nchini wengine ni chama cha kilichojipambanua kipagania maslahi ya wafanyakazi na wakulima NRA pamoja na ADA TADEA ambapo kupitia mgombea urais wa chama hicho John Shibuda amesema mbali na ungwe hii kukamilika amewataka wasimamizi wa uchaguzi kusimamia uchaguzi kulingana na katiba na si matakwa ya watu binafsi.
Soma zaidi: NEC yasema maandalizi ya uchaguzi Tanzania yaendelea vyema
Ikiwa zimesalia saa chache kukamilika kwa zoezi la kuwapitisha wagombea urais takriban vyama kumi na tatu bado havijathibithishwa wagombea wake wa nafasi ya urais na NEC endapo wamekidhi vigezo, ambapo hadi sasa vyama vilivyowasili katika ofisi za tume hiyo vikisubiri kuthibithishwa ni pamoja na chama kikuu cha upinzani Chadema, NCCR Mageuzi pamoja na chama cha wananchi CUF.