1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maalim Seif awekewa pingamizi kuwania urais wa Zanzibar

Mohammed Khelef
11 Septemba 2020

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilitangaza kuwaruhusu wagombea 16 wa urais wa Zanzibar kuanza kampeni zao tarehe 11 Septemba, lakini iliacha kumpitisha mgombea wa chama cha ACT-Wazalendo kwa sababu ya kuwekewa pingamizi.

Sansibar Maalim Seif Sharif Hamad CUF Präsidentschaftskandidat
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Ingawa siku ya Ijumaa (Septemba 11) ndiyo iliyotangazwa rasmi kuwa mwanzo wa kampeni za urais wa Zanzibar, uwakilishi na udiwani, hali haikuwa hivyo kwa wagombea kadhaa wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, akiwemo mgombea na mwanasiasa mashuhuri kwenye visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi, Maalim Seif Sharif Hamad, ambao wameekewa pingamizi na wagombea wenzao.

Wakati Maalim Seif aliwekewa pingamizi na wagombea urais wa vyama viwili visivyofahamika sana vya upinzani, Democratic Party (DP) na Demokrasia Makini, wagombea wake wa uwakilishi na udiwani waliwekewa pingamizi zaidi na wenzao wa chama kinachotawala, CCM.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Maalim Seif alipingwa kwa sababu "miongoni mwa fomu zake za kuomba uteuzi zilikuwa na makosa", kwa mujibu wa waweka pingamizi. 

Wapinzani walalimikia rafu za mapema

Hadi majira ya saa 4:00 usiku wa Alkhamis (Septemba 10), hakukuwa na muafaka kwenye kikao cha kujadiliana pingamizi hilo katika Ofisi za ZEC zilizopo Maruhubi, kando kidogo ya kitovu cha Mji Mkongwe wa Zanzibar, na suala hilo lilipelekwa mbele, pakitarajiwa uamuzi wake kutoka leo (Ijumaa, Septemba 11). 

Maalim Seif Sharif Hamad (kulia) akiwa na mgombea urais wa Tanzania kupitia chama chake cha ACT Wazalendo, Benard Membe.Picha: DW/E. Boniphace

Hayo yakijiri, wagombea wengine kadhaa wa nafasi za uwakilishi na udiwani wa chama hicho nao pia hawakukabidhiwa vyeti vya uteuzi na ZEC, baada ya kujulishwa kwamba wamewekewa pingamizi na wenzao kutoka CCM.

Chama cha ACT-Wazalendo kinalalamika kuchezewa rafu kwenye uchaguzi huu, ambapo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari siku ya Jumatano (Septemba 9), Naibu Katibu Mkuu Nassor Mazrui, alionya dhidi ya kile alichokiita "njama ovu za kuwaenguwa wagombea" wa chama chake.

Katika wilaya nzima ya Magharibi, kwa mfano, wagombea wote wanne wa uwakilishi na madiwani wao waliwaambia waandishi wa habari kuwa waliarifiwa kuhusu pingamizi na maafisa wa ZEC majira ya saa 11:00 jioni, ikiwa ni saa nzima tangu kumalizika kwa muda rasmi wa kuweka pingamizi. 

Kampeni zaanza rasmi

Wakati Maalim Seif na wagombea wengine wa chama chake wakiwa hawajui hatima ya pingamizi dhidi yao na endapo wataruhusiwa kuwania, kampeni rasmi za uchaguzi wa Oktoba 27 na 28 zimeanza visiwani humo, ambapo chama kidogo cha ADC kilitazamiwa kuzinduwa kampeni zake za urais kisiwani Unguja.

Hata hivyo, kama zilivyo siasa za Zanzibar, ni vyama viwili tu ndivyo vinavyotazamiwa kutunishiana misuli kwenye uchaguzi huu - chama kinachotawala cha CCM, ambacho kilitangaza kuanza kampeni zake siku ya Jumaamosi (Septemba 12).

Bado haijafahamika kuhusu ACT Wazalendo ambayo kwa sasa inapigania kurejea kwenye uchaguzi. 

Wazanzibari wengi masikio yao wameyaelekeza kwa ZEC ambayo ilitarajiwa kuendelea kuyasikiliza mapingamizi dhidi ya wagombea hao na kutoa uamuzi wake kabla ya jioni ya Ijumaa.

Imeandikwa na Salma Said, DW Zanzibar na Mohammed Khelef, DW Bonn