1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya Ulaya kuususia kwa kiasi Urais wa EU wa Hungary

16 Julai 2024

Tume ya Ulaya imesema itasusia kwa kiasi fulani urais wa zamu wa Hungary wa Umoja wa Ulaya kutokana na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban kujiamulia kufanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Orban alipomtembelea Putin mjini Moscow
Ziara ya Orban katika miji ya Kyiv, Moscow, Beijing, Washington na Mar-a-Lago, Florida mwezi huu, mara baada ya Hungary kuchukua Urais wa Umoja wa Ulaya, ililaaniwa vikali na washirika wa Ulaya.Picha: Valeriy Sharifulin/SNA/IMAGO

Baraza kuu la Umoja wa Ulaya mjini Brussels limechukua hatua hiyo ya kususia kwa kiasi fulani urais wa umoja wa ulaya wa zamu unaoshikiliwa na Hungary kwa muhula wa miezi sita kuonesha kutoridhika na ziara za Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbanambazo alizitaja kama ni "ujumbe wa amani" alizofanya mara tu baada ya kuchukua nafasi hiyo mwanzoni mwa mwezi huu.

Soma Pia: Je, Orban atafanikisha nia yake ya kutatua mzozo wa Ukraine? 

Hungary imesema Brussels inabagua wakati hatua ya urais wa zamu ni haki sawa kwa nchi wanachama zote zinaposhika usukani wa kuiedhesha jumuiya hiyo.

Kushoto: Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban. Kulia Donald TrumpPicha: Carlos Barria/REUTERS

Katika siku za kwanza za urais wa Hungary, rais huyo mpya wa Umoja wa Ulaya Viktor Orban alizitembelea Ukraine, Urusi, China na nchini Marekani kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa jumuiya ya kujihami ya NATO, na baada ya hapo alikwenda kukutana na rais wa zamani wa Marekani na mgombea wa urais katika uchaguzi ujao Donald Trump katika mji wa Florida.

Safari yake ya mjini Kiyv ilikuwa ya kwanza tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, licha ya kwamba nchi yake Hungary inapakana na Ukraine.

Nchi kadhaa wanachama zinazopakana na Urusi tayari zimechukua hatua ya kuisusia Hungary. Serikali ya Sweden wiki iliyopita ilitangaza kuwa, Finland, Estonia, Latvia, Lithuania na Poland hazitawapeleka mawaziri wake kwenye mikutano ya mwezi huu wa Julai chini ya urais wazamu wa Hungary wa Umoja wa Ulaya hatua ambayo inaashiria kupinga mazungumzo ya Orban na Putin huko mjini Moscow.

Kushoto: Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban alipomtembelea Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy mjini KiyvPicha: Maxym Marusenko/Nur Photo/IMAGO

Hata hivyo Hungary ilikosolewa vikali na nchi zingine wanachama wa Umoja wa Ulaya na pia washirika waNATO.

Waziri wa Sweden anayehusika na Masuala ya Umoja wa Ulaya Jessika Roswal, amesema wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya pia wanazingatia kuchukua hatua kama hizo.

Ziara zake hizo kwa jina "ujumbe wa amani” Viktor Orban anajaribu kujionyesha kama mmoja wa kati ya wakuu wachache sana wa serikali za nchi za Umoja wa Ulaya na katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO ambao bado wanaweza kufanya mazungumzo yenye tija na Urusi.

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen Picha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Eric Mamer, msemaji wa Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamelaani safari hiyo na kusisitiza kwamba Orban hakuridhiwa na Umoja wa Ulaya kufanya mazungumzo ya amani.

Msemaji huyo Eric Mamer pia ametangaza kwamba Tume ya Ulaya itavunja utamaduni wa viongozi wake kuhudhuria hafla ya kumkaribisha rasmi rais mpya wa zamu wa Umoja wa Ulaya ambapo mara hii utafanyika nchini Hungary kwa ajili ya kumakaribisha Waziri Mkuu Viktor Orban atakayekalia kiti hicho kwa muda wa miezi sita.

Hatua ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kususia hafla hiyo ni pigo kwa rais mpya wa Umoja wa Ulaya Viktor Orban.

Soma Pia: Xi: Mataifa yenye nguvu fanikisheni amani Urusi na Ukraine 

Waziri wa Hungary wa Masuala ya Umoja wa Ulaya, János Bóka, amesema uamuzi wa tume ya Ulaya sio sahihi. Ameandika kwenye mtandao wa X kwamba Tume ya Ulaya ni taasisi ya Umoja wa Ulaya na kwa hivyo Tume hiyo haiwezi kubagua kwa kuchagua taasisi au nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya inayotaka kushirikiana nazo. Na ameuliza Je, maamuzi yote ya Tume ya Ulaya sasa yanatokana na masuala ya kisiasa?

Vyanzo: DPA/ https://www.dw.com/en/european-commission-to-partly-boycott-hungarys-presidency/a-69674726

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW