Tunisia kufanya uchaguzi wa bunge Jumapili
24 Oktoba 2014Baada ya wiki tatu za kampeni za chini kwa chini, Tunisia iko tayari kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa mara ya pili tangu uchaguzi wa 2011, utakaoanza na uchaguzi wa bunge tarehe 26 Oktoba na kufuatiwa na uchaguzi wa rais tarehe 23 Novemba.
Zaidi ya wananchi milioni tano imeripotiwa kuwa wamekamilisha masharti ya kupiga kura na wanangoja kuchagua wabunge 217 ambao wanajumuisha wagombea wa chama cha kiislamu cha Ennahda pamoja na vyama vyengine kadhaa vya siasa.
Katika mahojiano ya televisheni mwishoni mwa wiki hii Rais wa Tunisia Moncef Marzouki, ameuita uchaguzi wa rais na wa bunge kuwa ni hatua muhimu katika siasa za Tunisia. Na huku kiongozi wa chama cha kisilamu cha Ennahda Ghannouchi, ametabiri kuwa chama hicho kitachota kura nyingi zaidi ya ile asilimia 37 iliyopatikana kwenye uchaguzi uliopita.
Jumuiya ya kimataifa imeitolea mfano serikali ya muungano wa Tunisia ambayo inaongozwa na chama cha Ennahda kikisaidiwa na vyama vyengine viwili vya kisiasa.
Tunisia imeshuhudia utulivu tangu maandamano ya vuguvugu ya msimu wa mchipuko ya mwaka 2011, tofauti na vurugu zinazoendelea mataifa mengine ya kiarabu ikiwamo Libya, Yemen, na Syria.
Waziri mkuu wa zamani wa Tunisia Ali Larayedh amesema, "Ukilinganisha Tunisia na mataifa mengine ya kiarabu yaliyoshuhudia maandamano ya msimu wa mchipuko, basi sisi tunachukuliwa kuwa ni mfano ulioonyesha mafanikio, kwa mtazamo wa ulinzi wa uhuru na demokrasia."
Kwa mujibu wa Rached Ghannouchi kiongozi wa chama cha Ennahda, chama hicho kimekubaliwa na wengi na ni chama pekee kilichoweza kuanzisha hali ya kidemokrasia nchini humo. Lakini wadadisi wa chama cha siasa cha Nidaa Tounes, walipinga hayo na kusema chama hicho kimeonesha utekelezaji mbovu juu ya masuala ya usalama na mageuzi ya kiuchumi.
Tunisia yakabiliwa na changamoto kubwa
Ingawa Tunisia imeweza kujitoa katika mtikisiko unaondelea ndani ya mataifa kadhaa ya Kiarabu, wachambuzi wanasema bado ni mapema mno kutathmini kama kweli nchi hiyo imeshafanikiwa kidemokrasia.
Licha ya kuwa uchaguzi huo wa bunge unaotarajiwa kufuatiliwa kwa karibu na jumuiya ya kimataifa, wananchi wengi wa Tunisia wamesema hawatokwenda kupiga kura.
Kamal Torkhani mmjoja kati ya maelfu ya wanachi walioshiriki katika mapinduzi ya Tunisia ya mwaka 2011 amesema yeye hatokwenda kupiga kura siku ya Jumapili, na aliongeza kwa kusema na nina mnukuu "Pale tutakapokuwa na wanasiasa waaminifu ambao wanajali matatizo ya wananchi, basi nami nitakwenda kupiga kura,"mwisho wa kumnukuu. Kamal aliongeza kusema, " Wananchi bado tunaishi chini ya shinikizo la serikali. Kama binadamu, hatuna hadhi wala haki."
Miongoni mwa vijana wa Tunisia, wengi wanaoneka kukosa shauku ya kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao, ingawa wanaonesha wazi kuwa wanajali sana mustakabali wa nchi yao.
Kwa mtazamo wake Amal Halbaouti, kijana wa miaka 23, amesema "Hatutaki Tunisia kurudi kule ilipotoka siku za uongozi wa rais wa zamani Ben Ali lakini pia tunahitaji maisha bora zaidi ya haya tuliyonayo."
Mwandishi: Yusra Buwayhid/AFPE
Mhariri: Josephat Charo