Tunisia mambo bado
24 Januari 2011Wiki hii inaelekea ya kufuzu au kuanguka kwa serikali ya mpito iliyoundwa wiki iliopita na ambayo inawajumuisha pia waliokua wapinzani wa rais Ben Ali aliyekimbilia Saudi Arabia. Chama kikuu cha wafanyakazi nchini humo, UGTT, kimekataa kuitambua serikali mpya kwa sababu nyadhifa muhimu zimo mikononi mwa wafuasi wa utawala ulioangushwa, akiwemo Waziri Mkuu Mohammed Ghannouchi.
Raia wengi wa Tunisia wana msimamo huo huo na wamekua wakiandamana kila siku tangu serikali hiyo ilipotangazwa Jumatatu iliopita, huku wakidai pia kuvunjwa kwa chama cha Ben Ali cha RCD, ambacho kimetawala Tunisia kwa miongo kadhaa.Shule kadhaa zimefungwa kwa sababu ya mgomo uliotishwa na waalimu kuipinga serikali mpya.
Waandamanaji ambao baadhi wanasema walitembea mwendo wa kilomita 80 kufika mji mkuu, walibeba picha za kijana Mohamed Bouazizi aliyejichoma moto na kufariki dunia, baada ya kunyanyaswa na polisi wakati akijaribu kufanya biashara ya matunda. Tukio hilo likawa chanzo cha vuguvugu la umma kupinga kuzidi kwa umasikini na ukosefu wa kazi, lililomsababishia hatimaye Rais Ben Ali kukimbilia Saudi Arabia. Bouazizi alikua amehitimu chuo kikuu lakini hakupata ajira.
Waandamanaji hao wanadai wataendelea klubakia majiani hadi serikali hiyo ya mpito nayo imeanguka na wahusika wamekimbia kama alivyofanya kinara wao Ben Ali.
Jana serikali ilitangaza kukamatwa kwa wasdhirika watatu wa Ben Ali akiwemo Rais wa baraza la Seneti Abdullah Kalal . Pia mkuu wa kituo cha binafsi cha televisheni Hannibal TV ametiwa nguvuni Matangazo ya kituo hicho yalikatika ghafla na baadae kutokeza matangazo mengine yakitanguliwa na nembo mpya isemayo "Sauti ya Umma." Awali maafisa walisema wamewakamata pia watu 3, jamaa wa Ben Ali na mali zao zote zimezuiliwa.
Mjini Paris Rais wa Ufaransa Nikolas sarkozy amekiri leo kwamba awali nchi yake ilishindwa kufahamu kiwango cha hasira za watunisia dhidi ya utawala wa Ben Ali. Akizungumza na waandishi habari leo, Sarkozy alikiri kwamba nchi yake ilichelewa mno kuzungumzia matukio nchini Tunisia, lakini akasema ilimbidi awe muangalifu asionekane anaingilia mambo ya ndani ya taifa hilo.
Ufaransa imekosolewa vikali kwa kuunga mkono utawala wa kimabavu wa Ben Ali kwa muda mrefu na wadadisi wanayaangalia matamshi hayo ya Sarkozy kuwa ni kujitoa kimasomaso tu.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/AFP
Mpitiaji: Abdul Mtullya