Tunisia yaanza maombolezo
21 Januari 2011Maombolezo haya ya siku tatu ni kwa ajili ya watu 78, ambao maafisa wa Tunisia wanasema waliuliwa na vikosi vya usalama vilivyokuwa vikijaribu kuyazuia maandamano ya umma yaliyoanza katikati ya mwezi Disemba mwaka jana na kusababisha Ben Ali kukimbia nchi katikati ya mwezi huu. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unakisia kuwa waliokufa kwenye mkasa huu wa mwezi mmoja wanafikia hadi watu 100.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana, baada ya kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri, serikali ya mpito imesema kwamba, maombolezo haya ni kwa heshima ya wale wote waliojitolea kuleta ukombozi mpya kwa taifa lao.
Mapema, Rais Fouad Mebazaa alikuwa ametamka hadharani, kuyatambua mapinduzi yaliyofanywa na wananchi wa Tunisia kama hatua ya kishujaa; na akaahidi kwamba uongozi wake utajitenga mbali kabisa na yale yote yaliyowafanya Watunisia kuingia barabarani na kuipindua serikali yao.
Mwanzo mwema
Na katika kile kinachoonekana kama mwanzo mwema, serikali hiyo ya mpito imethibitisha muswaada wa sheria, ambao unatoa msamaha kwa wafungwa wote wa kisiasa, waliokamatwa chini ya utawala wa miaka 23 wa dikteta Ben Ali.
Hata hivyo, watu bado wanalalamika kuwa uachiliwaji wa wafungwa hao unakwenda kwa kasi ndogo, huku wengi wa wale waliowekwa kwenye jela za Ben Ali bila ya sababu za msingi wakiendelea kubakia huko.
"Mwanangu Ziad, walikuja nyumbani na kumchukua. Wakamfunga miaka mitano na walimtesa sana hadi akakaribia kufa. Aliteswa na kwa hivyo tumeteseka pamoja naye. Hadi sasa hawajamtoa na tayari ameshatumikia miaka mitatu na miezi mitano. Wako wapi hapo watu walioachiliwa?" Anasema mmoja wa wazazi ambao watoto wao bado wanasota kwenye jela za Ben Ali.
Kwa upande mwengine, serikali ya Mebazaa imeagiza kushikiliwa kwa mali zote za chama cha Ben Ali, Constitutional Democratic Rally, RCD, ambacho Mebazaa na Waziri wake Mkuu, Muhammad Ghannouchi juzi waliamua kukihama, na ambacho sasa uongozi wake mzima umesambaratika.
Mawaziri wengine, nane waliokuwa wanachama wa chama hicho, nao walitangaza hapo jana kukiacha mkono, katika jitihada zao za kujtenga na kivuli cha utawala wa kikatili wa Ben Ali.
Mipango ya uchaguzi mpya
Leo hii, serikali inatarajiwa kutangaza mpango wa uchaguzi mpya wa rais na wabunge, utakaofanyika ndani ya miezi sita ijayo, licha ya kwamba sheria inataka uchaguzi uitishwe ndani ya miezi miwili tu.
Lakini kiongozi wa zamani wa chama cha Kikomunisti cha Ettajdid, ambaye sasa ni mjumbe wa baraza la mawaziri, ameliambia Shirika la Habari la AFP kwamba, si rahisi kuitisha uchaguzi ndani ya miezi miwili kwa kuwa kuna mambo mengi ya kufanywa, ikiwemo kuzipitia na kuziandika upya sheria.
Hata baada kiongozi huyo wa miaka 74 kuikimbia nchi, bado waandamanaji wameendelea kudai kumalizwa kwa mabaki yoyote ya utawala wa dikteta huyo yaliyosalia, kikiwemo chama chake cha RCD, kukamatwa kwa mali zake na hata kurudishwa yeye mwenyewe Tunisia kukabiliana na mkono wa sheria.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman