1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaTunisia

Tunisia yafanya uchaguzi wa Bunge uliosusiwa na upinzani

17 Desemba 2022

Raia wa Tunisia wanapiga kura siku ya Jumamosi kuchagua bunge jipya.

Tunesien Parlamentswahl | Wahllokal
Picha: Zoubeir Souissi/REUTERS

Uchaguzi huo unafanyika chini ya kiwingu cha mzozo wa kidemokrasia, hali ngumu ya uchumi na mfumuko mkubwa wa bei.

Vyama kadhaa vya upinzani ikiwemo muungano wa Salvation Front ambao unakijumuisha chama maarufu cha Ennahda vimeususisa uchaguzi huo kwa sababu vinasema ni sehemu ya mpango wa rais Kais Saied kuimarisha nguvu na madaraka yake.

Mmoja wa viongozi wa vyama vya upinzani nchini humo Ezzeddin Hazgui kutoka  amesema wanaususia uchaguzi huo kwa kuwa hawawezi kujiunga na mtu anayesambaratisha taasisi za dola.

Uamuzi wa kususia uchaguzi huo yumkini utapelekea bunge lijalo kuwa na wanasiasa watiifu kwa rais Saied ambaye wakosoaji wake wanamtuhumu kuchukua mwelekeo wa udikteta.

Wagombea 1,500 wanawania viti vya Bunge la Taifa

Rais Kais Saied wa Tunisia akipiga kura katika uchaguzi wa Bunge Picha: Tunisian Presidency via REUTERS

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema saa mbili asubuhi saa za Tunisia na vilitarajiwa kufungwa jioni ya saa kumi na mbili.

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi vyama vitano na wagombea 1,500 wameidhinishwa kuwania nafasi za bunge.

Idadi ya wapiga kura waliojitokeza mnamo mapema asubuhi ilikuwa ndogo ingawa waandishi wa Shirika la Habari Associated Press wamearifu kuwa walishuhudia misusuru ya watu kwenye vituo kadhaa mjini Tunis.

Rais Kais Saied na mkewe Ichraf Chebil, walipiga kura huko Ennasr kitongoji cha nje kidogo ya mji mkuu Tunis.

Je, utawala wa mabavu unanunia Tunisia? 

Uchaguzi kwenye taifa hilo la Afrika Kaskazini unafanyika wakati kuna hisia za wazi za kuporomoka kwa imani ya umma wa Tunisia kwa utawala wa rais Kaes Saeid na ajenda yake ya kuufanyia mageuzi mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Picha: Chedly Ben Ibrahim/NurPhoto/picture alliance

Kiongozi huyo aliyechaguliwa kuwa rais wa Tunisia miaka miwili iliyopita alianza vitimbi katikati ya mwaka uliopita kwa kutangaza kusitisha shughuli za Bunge la Taifa na kumtimua waziri mkuu wa wakati huo Hichem Mechichi.

Mnamo Februari mwaka huu alisitisha kazi za Baraza la Mahakama ya Juu ya nchi hiyo na mwezi mmoja baadaye akatangaza kulivunja kabisa bunge la Tunisia.

Hakuishia hapo, aliitisha kura ya maoni mnamo Julai mwaka huu kuifanyia marekebisho katiba ya Tunisia ambayo yanamwongezea nguvu za kutowajibika kokote.

Sheria za uchaguzi za nchi hiyo pia zilibadilishwa mwezi Septemba na ndiyo zitatumika kuongoza uchaguzi unaofanyika leo.

Nafasi za majimbo zimepunguzwa kutoka 217 hadi 161 na kwa mara ya kwanza rais wa Tunisia wanachagua wagombea mmoja mmoja badala ya kuvipigia kura vyama vya siasa.

Masuala yote hayo yamejenga msingi wa uchaguzi wa leo kukosa sura ya uhalali miongoni mwa wadau wa siasa wa nchi hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW