1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia yaonya kuhusu uchumi wake kuporomoka

Josephat Charo
1 Juni 2021

Wanasiasa na maafisa wa Tunisia wanaonya kuhusu uchumi kuporomoka ikiwa serikali haiwezi kukubaliana juu ya mpango mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF msimu huu wa kiangazi.

Tunesien | Coronavirus | Ausgangssperre
Picha: Wassim jdidi/PanoramiC/imago images

Watunisia wamezowea mazungumzo ya dakika za lala salama yanayohusu matakwa ya wakopeshaji wa kigeni dhidi ya maoni ya umma, lakini safari hii mvutano wa kung'ang'ania madaraka kati ya rais, waziri mkuu na bunge umeongeza changamoto mpya.

Katika mahojaino na shirika la habari la Reuters waziri mkuu wa zamani Youssef Chahed alisema hali ya kisiasa nchini Tunisia imekwama na kwamba hakuna mjadala wa maana unaoendelea miongoni mwa wanasiasa kuhusu kuuimarisha uchumi.

Kufuatia janga la COVID-19 kupuguza uzalishaji kwa asilimia 8.8 mwaka uliopita na kuliongeza deni la taifa kufikia asilimia 91 ya pato jumla la taifa, hali ni tete na ya dharura.

Gavana wa benki kuu Marouan Abassi aliliambia bunge kwamba ikiwa serikali itajaribu kuitumia benki hiyo kulipia nakisi hiyo badala ya kukubali mkopo wa shirika la fedha la kimataifa IMF, mfumuko wa bei utaongezeka kwa kiwango kikubwa kama ilivyotokea nchini Venezuela.

Waziri wa zamani wa fedha Hakim Hamouda ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mzozo huo unatishia kulifilisi dola. Waziri wa zamani aliyehusika na masuala ya mageuzi, Taoufik Rajhi, ambaye aliongoza mazungumzo kuhusu mpango wa awali wa IMF kwa ajili ya Tunisia ameyaeleza mazungumzo ya sasa kuwa fursa ya mwisho kuepusha uchumi kuanguka. Viongozi wote wawili wameonya Tunisia huenda ikakabiliwa na hatima kama ile ya Lebanon, ambako sarafu imeporomoka thamani yake na hazina ya taifa haina kitu, hali iliyozusha machafuko ya kijamii.

Shughuli nyingi zilifungwa kufuatia vizuizi vya kukabiliana na coronaPicha: Yassine Gaidi/AA/picture alliance

Mpango wa IMF huenda ukasaidia kupatikana msaada zaidi wa kifedha kusaidia kuimarisha ufanisi wa maandamano ya msimu wa machipuko ya kiarabu na mshirika muhimu wa Ulaya katika usalama na uhamiaji.

Bajeti ya Tunisia ya mwaka 2021 inakadiria mahitaji ya mkopo wa thamani ya dola bilioni 7.2, ikiwemo mikopo ya takriban dola bilioni 5. Ulipaji madeni umewekwa katika dola bilioni 5.8 ukiwemo mkopo wa dola bilioni moja unaotakiwa kulipwa mwezi Julai na Agosti.

Mazungumzo ya IMF yanatarajiwa kuendelea msimu wote wa kiangazi. Waziri Mkuu Hichem Mechichi ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba anataka dola bilioni 4, ingawa watu wachache wanafikiri kiwango chochote zaidi ya dola bilioni 3 huenda kikatolewa.

Mkataba wa pande hizo mbili huenda ukahitajika kuiwezesha Tunisia kulipa deni lake msimu wa kiangaizi. Wanasiasa wa Tunisia wanasema kibinafsi kwamba Qatar au Libya huenda zikatoa fedha.

Wanadiplomasia wanasema ari ya kimataifa kwa Tunisia huenda ikawa na mchango muhimu katika mazungumzo, lakini wanakatishwa tamaa na kile wanachokiona kuwa ni matumizi mabaya ya fedha na shirika la IMF linaitaka Tunisia ifanye mageuzi ya maana.

Chahed amesema msaada wa kigeni hasa nchini Marekani na Ufaransa umepiga jeki fursa ya kupatikama makubaliano, lakini ikiwa Tunisia itaahidi kufanya mageuzi.  Hata hivyo mageuzi makuu ya msingi - kupunguza ruzuku, kuyafanyia mageuzi makampuni yanayomilikiwa na serikali na kupunguza gharama ya mishahara ya wafanyakazi wa umma - yanapingwa na chama cha wafanyakazi cha UGTT na baadhi ya vyama vya kisiasa ambao wanasema Watunisia wamechoshwa na kujitolea kusikoisha.

Hali ya umma kutoridhika iliyodhihirika katika uchaguzi wa mwaka 2019 kwa kukataliwa wanasiasa wenye haiba kubwa na hivi karibuni maandamano ya mwezi Januari huenda yakagubika hatua za kushughulikia changamoto za kiuchumi.

Mivutano ya aina hii ya ndani itaifanya vigumu kwa serikali kulihakikishia shirika la IMF na wakopeshaji wengine wa kigeni kwamba inaweza kutekeleza mageuzi yoyote inayoyaahidi.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW