1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, maandamano ya vijana yatabadili siasa za Tunisia?

Hawa Bihoga
23 Septemba 2024

Nchini Tunisia kuna shuhudiwa msako mkali dhidi ya wapinzani wa kisiasa, nao vijana wameanza kuingia mitaani kupinga kile wanachokiita ubabe wa rais alieko mamlakani Kais Saied.

Tunisia | Waandamanaji wakishinikiza matakwa yao.
Waandamanaji nchini TuniasiaPicha: Yassine GaidiAnadolu/picture alliance

Maandamano hayo ni makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa kipindi cha miaka kadhaa, ambapo makumi kwa maelfu ya vijana wa Tunisia wakiingia katika mitaa ya mji mkuu Tunis.

Makundi hayo ya vijana pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu na kisiasa wanamshutumu rais Kais Said kwa kuimarisha utawala wa kimabavu na kuuzika ushindani wa kisasa wiki mbili tu kabla ya uchaguzi wa rais.

May Abidi ambae ni kijana ameshindwa kuzuia hasira zake na kujiunga na vuguvugu la asasi za kiraia na vyama vya siasa wakionesha hofu yao inayoongezeka dhidi ya mamlaka ya rais Kais, ameiambia DW wanachokitaka kwa sasa ni uchaguzi wa kidemokrasia kama ilivyokuwa mwaka 2019.

Mnamo 2019 raia walitoa wito wa mabadiliko baada ya mawaziri tisa kushindwa kutatua matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa ajira na rushwa inayopigiwa kelele katika taifa hilo la Afrika kaskazini.

Katika uchaguzi wa rais 2019- wa kwanza baada ya vuguvugu la 2011 lililomwondoa dikteta wa muda mrefu Zine El Abidine Ben Ali ambae ni profesa wa zamani wa sheria na mgombea binafsi Kais Saied akipata ushindi wa kishindo kwa asilimia 72 ya kura.

Soma pia:Makumi ya wanachama wa Ennahda wakamatwa kuelekea uchaguzi Tunisia

Aliahidi kukabiliana na ufisadi, kurekebisha nchi iliyozongwa na matatizo kadhaa na kutoa mustakabali wenye matumaini kwa vijana, lakini miaka mitano baadae mambo yamekwenda mrama.

Mbinyo wa kisiasa unazidi kushuhudiwa na hali mbaya ya uchumi wa nchi, ambapo kiwango cha ukosefu wa ajira kwa sasa ni asilimia 39 kwa vijana. Nabil Hajji kiongozi wa chama cha Attayar amesema Rais said hata kubali uchaguzi ambao hautamuhakikishia ushindi.

"Leo hii ikiwa  rais yeyote alioko mamlakani angelikuwa na imani kwamba wananchi bado wanamuhitaji kwenye mamalaka asingelifanya ukiukwaji wa kiwango hiki." Alisema mwanasiasa huyo.

Aliongeza kwamba "angeliamini kwamba angelishinda kwenye sanduku la kura. Kwa sasa iko wazi kwamba hata Kais Saied mwenyewe anatambua kwamba amepoteza umaarufu wote."

Tunisia katika ramani ya demokrasia

Miaka miwili tu, baada ya rais Saied kuchaguliwa aliazimia kuunganisha mamlaka yake. Tangu Julai 2021 rais huyo amevunja vyombo vingi vya kidemokrasia na kuwafunga jela waandishi wa habari, wanasheria na hata wapinzani wa kisiasa.

Vuguvugu la wahamaji Kusini mwa Jangwa la Sahara

01:50

This browser does not support the video element.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani vikali kile inachokitaja dhuluma zinazoendelea ambazo zinatumika na rais kama rungu katika kupata muhula wa pili kwenye uchaguzi ujao wa Oktoba.

Kati ya wagombea 17 ambao walitangaza kuwania urais wagombea 14 walienguliwa ama kuzuiliwa. Hata hivyo tume ya uchaguzi Tunisia iliwathibitisha wagombea wawili pekee kupambana na Saied.

Soma pia:HRW: Mamlaka za Tunisia zawakandamiza wanaompinga rais Kaes

Siku ya Jumatano, mahakama katika mji wa kaskazini-magharibi wa Jendouba ilimtia hatianiani mmoja wa wagombea hao waliothibitishwa, Ayachi Zammel, ambae ni mkuu wa chama cha upinzani cha Azimoun, na kumhukumu kifungo cha miezi 20 jela kwa mashtaka yanayohusiana na kughushi saini za wapiga kura. Kulingana na wakili wake, amesema shutuma hizo hazina mshiko.

Wakosoaji wanasema Saied anatumia tume ya uchaguzi na mahakama kupata ushindi kwa kuzima ushindani na kuwatisha wagombea hatua inayofifisha demokrasia.

Rais Kais mara kadhaa amekuwa akikanusha shutuhuma hizo kwa kusema anapambana na wasaliti, mamluki na mafisadi katika taifa lake.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW