Tuzo ya uhuru wa vyombo vya habari , Merkel amtunza mchoraji wa Denmark Westergaard
9 Septemba 2010Katika kasri la Sanssouci mjini Potsdam, usiku wa jana kulifanyika hafla ya kumpa tuzo msanii wa katuni kutoka Denmark Kurt Westergaard, tuzo ya vyombo vya habari. Tuzo hiyo ilitolewa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Westergaard alichora moja kati ya vobonzo 12 vinavyomkejeli mtume Muhammad , ambapo miaka mitano iliyopita vilichapishwa katika gazeti la Denmark la Jyllands-Posten. Kibonzo alichokichora kinaonyesha mtume Muhammad akiwa na bomu katika kilemba alichovaa. Kuchapishwa kwa vibonzo hivyo katika mwaka huo 2005 kulichochea ghasia duniani kote katika ulimwengu wa Waislamu na kusababisha maandamano ya ghasia. Raia huyo wa Denmark amepata tuzo hiyo kwa kutambua mchango wake katika uhuru wa vyombo vya habari.
Baraza la ushauri la chama cha waandishi habari wa Potsdam lilitaka kuepusha hatari, na kuzuwia taarifa hizo , na kutangaza siku ya tarehe 6.9, Jumatatu, mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka huu 2010, kuwa ni mchora vibonzo raia wa Denmark Kurt Westergaard, kutokana na msimamo wake usio yumba kwa ajili ya vyombo vya habari na uhuru wa mawazo pamoja na ushujaa wake wa kulinda thamani ya demokrasia licha ya ghasia na vitisho vya kuuwawa.
Westergaard, anayeishi hadi sasa katika ulinzi wa polisi tangu pale vibonzo hivyo vilipochapishwa, hakutaka kujiweka katika hatari katika hafla hiyo mjini Potsdam. Kwa hiyo kasri hilo la Sanssouci liliwekewa ulinzi mkali na shughuli ya kukabidhi tuzo hiyo ilifanyika katika hali ya ulinzi mkali.
Mwanachama wa chama cha waandishi habari wa Potsdam na mhariri mkuu wa gazeti linalosambazwa kwa wingi nchini Ujerumani la Bild, Kai Diekman alikuwa na haya ya kusema.
Nadhani hapa sio suala la hatari ya usalama, hili ni suala la udhibiti wa kimbinu, ndio sababu kuna hali kama hii, ni ishara ya kwamba kile ilichokisababisha katuni hizo hakikuleta hali nzuri. Na mtu hapaswi kuweka msisitizo zaidi.
Gazeti la Bild kwa mfano liliamua wakati ule, kutochapisha vibonzo hivyo. Lakini kile kilicho muhimu kwetu sisi, ni kwamba tuko katika bara la Ulaya na kwamba sheria lazima zifuatwe .
Ameongeza kuwa hakubaliani na yeyote atakayeeleza tofauti na hivi. Lakini yuko tayari kutoa maisha yake kwa kile mchoraji alichoweza kukisema.
Na msimamo huo umeonekana katika hafla ya jioni ya jana.
Hotuba kuu ilitolewa na kansela wa Ujerumani Anfela Merkel katika halfa hiyo mjini Potsdam. Hotuba yake ilisisitiza zaidi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kutoa mawazo. Na amemtetea sana Westergaard. Kama mchoraji alipaswa kufanya kazi yake.
Haijalishi iwapo vibonzo vyake tunavipenda ama la, iwapo tunapaswa na kwamba tunamsaidia ama hapana. Ana weza kufanya hivyo? Ndio anaweza. Yeye ni msanii , kama walivyo wengi katika bara la Ulaya. Ulaya ni mahala ambapo msanii anaruhusiwa kueleza chochote. Hakuna kitu kinacholeta mgongano, kwamba Ulaya ni mahali ambapo uhuru wa kuabudu na wa dini unaheshimiwa sana.
Wakati huo huo, kiongozi wa baraza kuu la Waislamu nchini Ujerumani Nadine Elyas amekosoa hatua hiyo ya kumpa tuzo msanii huyo wa kuchora vibonzo.
Chama cha waandishi habari wa Potsdam kinatoa tuzo hiyo kila mwaka katika mtazamo wa Ulaya na dunia, katika kusisitiza na kuacha alama za uhuru wa habari.
Mwandishi : Wagner, Jörg / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman.