Mashambulizi mawili ya wanajihadi yaua zaidi ya watu 30 Mali
8 Mei 2026
Mashambulizi mawili katikati mwa Mali yanayodaiwa kufanywa na wapiganaji wa jihadi wenye mafungamano na kundi la Al-Qaeda yamewaua zaidi ya watu 30. Hayo yamesemwa na vyanzo vya ndani nchini Mali kwa shirika la habari la AFP.
Mashambulizi hayo yametokea chini ya kipindi cha wiki mbili baada ya shambulio kubwa lililoratibiwa na wapiganaji wa jihadi na waasi katika maeneo ya kijeshi, ambayo yameitumbukiza nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika mgogoro mpya wa usalama.
Kwa mujibu wa vyanzo vya usalama ni kwamba mashambulizi hayo yanadaiwa kufanywa na Kundi linalounga mkono Uislamu (JNIM) katika vijiji vya Korikori na Gomossogou.
Jeshi la Mali limesema hapo jana kuwa limefanya operesheni iliyoyalenga makundi ya kigaidi yenye silaha" katika eneo hilo na takriban wapiganaji kumi na wawili "wameangamizwa" lakini bila kutoa maelezo ya kina.