1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TYRE : Israel yazidi kujipenyeza Lebanon

12 Agosti 2006

Vikosi vya Israel vimezidi kujipenyeza ndani zaidi kusini mwa Lebanon leo hii na kusonga mbele kuelekea Mto Litani wakati vikianza kutanuwa mashambulizi yao ya ardhini dhidi ya Hizbollah.

Vikosi vya Israel vimefikia kijiji cha Ghandouriyeh kama kilomita 11 ndani ya Lebanon huko kukiwa ni kuingia ndani kabisa mwa Lebanon katika vita vya mwezi mmoja ambavyo vimeshuhudia Israel ikiishambulia Lebanon kutoka angani na ardhini.

Hizbollah imekiri kusonga mbele huko kwa Israel lakini imesema wapiganaji wake wamekishambulia kikosi cha Israel huko Ghandouriyeh na kuuwa pamoja na kujeruhi wanajeshi kadhaa wa Israel.Katika maeneo mengine Hizbollah imesema imefanya mashambulizi kadhaa katika magari ya deraya ya Israel na kuharibu vifaru 16 pamoja na kusababisha maafa makubwa kwa wanajeshi wa Israel.

Umoja wa Mataifa unataraji mashambulizi ya ardhini ya Israel kumalizika katika kipindi kisichozidi masaa 48 na kikosi cha kulinda amani cha kimataifa kuanza kuwekwa kusini mwa Lebabon katika kipindi cha wiki moja hadi siku 10.

Akizungumzia maandalizi ya kuwekwa kwa kikosi hicho mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa amani ya Mashariki ya Kati Alvaro de Soto amesema mjini Jerusalem kwamba mashambulizi ya Israel yako katika hatua za mwisho na kwamba yatamalizika katika kipindi cha siku moja hadi mbili.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert imesema kwamba usitishaji wa mapigano unaweza kuanza hapo Jumatatu lakini taarifa hiyo inapingana na kauli ya Mkuu wa Majeshi wa Israel Luteni Generali Dan Halutz ambaye amesema vikosi vya Israel vitaendelea na mashambulizi yake nchini Lebanon hadi hapo vikosi vya kimataifa vitakapowasili.

Azimio lililoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana linataka kukomeshwa kwa mapigano nchini Lebanon kati ya Israel na Hezbollah na uwekaji wa wanajeshi 15,000 wa Umoja wa Mataifa watakaosaidiwa na wanajeshi wa Lebanon wa idadi kama hiyo kudhibiti eneo la kusini mwa Lebanon wakati vikosi vya Israel vilivyolikalia kwa mabavu eneo hilo vitakapoondoka.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW