1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UAE yaharibu kombora lililorushwa na waasi wa Kihouthi

31 Januari 2022

Umoja wa Falme za Kiarabu umeharibu kombora lililorushwa na waasi wa Kihouthi nchini Yemen wakati wa ziara ya rais wa Israel Isaac Herzog nchini humo siku ya Jumatatu. Hakuna aliyejeruhiwa katika shambulizi hilo.

Yemen Huthi Kämpfer
Picha: Hani Mohammed/AP Photo/picture-alliance

Shirika la habari la WAM la Umoja wa Falme za Kiarabu limenukuu wizara ya ulinzi ya nchi hiyo ikisema kuwa vikosi vya ulinzi wa anga vilinasa na kuharibu kombora lililorushwa na kundi hilo la waasi wa Kihouthi. Wizara hiyo imeongeza kuwa ilijibu kwa kuharibu eneo la kurushia kombora hilo la Al-Jawf nchini Yemen dakika 30 baada ya kunasa kombora hilo. Aidha, izara hiyo imesema kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu unathibitisha kuwa tayari kukabiliana na vitisho vyovyote na utachukuwa mikakati ya kulinda taifa hilo dhidi ya mashambulizi ya aina yoyote.

Wakati huo huo, msemaji wa kundi hilo la Kihouthi Yahya Saree, amesema walirusha makombora ya Zulfiqar kuelekea Abu Dhabi na ndege zisizo na rubani huko Dubai. Saree amesisitiza onyo kwa wakazi na makampuni kukaa kando na makao makuu na taasisi muhimu za Umoja huo wa Falme za Kiarabu unaojivunia kuwa eneo salama la kibiashara na kivutio cha utalii wa kimataifa. Mamlaka ya Umoja wa Falme za Kiarabu imesema kuwa tukio hilo halikuwa na athari katika mpangilio wa safari za ndege huku safari hizo zikiendelea kama kawaida.

Isaac herzog - Rais wa IsraeliPicha: Jon Gambrell/AP Photo/picture alliance

Wiki iliyopita, afisa mmoja mkuu katika taifa hilo la kifalme, aliapa kwamba mashambulizi ya waasi wa Kihouthi hayatakuwa matukio ya kawaida kwa taifa hilo. Kombora hilo la waasi la hivi karibuni karibuni zaidi limerushwa wakati rais Isaac Herzog akifanya ziara ya kwanza katika Umoja wa Falme za Kiarabu kama rais wa kwanza wa Israel  baada ya mataifa hayo mawili kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia chini ya makubaliano ya Abraham ya mwaka 2020 yaliyosimamiwa na Marekani.

Rais Herzog, aliyekutana na mwanamfalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed Al-Nahyanh siku ya Jumapili, alitembelea eneo la maonyesho ya Dubai ya mwaka 2020 siku ya Jumatatu. Pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu na kiongozi wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al-Maktoum.

Ofisi ya Herzog imesema kuwa ataendelea na ziara yake kama ilivyopangwa huku Marekani ikishtumu shambulizi hilo la Kihouthi. Katika ujumbe kupitia mtandao wa twitter, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Ned Price, amesema kuwa wakati rais huyo wa Israeli anazuru Umoja huo kusuluhisha tofauti na kuimarisha uthabiti katika eneo hilo lote, waasi wa Kihouthi wanaendelea kufanya mashambulizi yanayowatishia raia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW