UAE yakanusha kutuma silaha Sudan
14 Agosti 2023Ghasia zinaripotiwa kuzuka upya kwenye mji wa Nyala na maeneo mengine ndani ya jimbo hilo la magharibi mwa Sudan siku ya Jumapili (Agosti 13).
Mapigano kati ya jeshi rasmi na wanamgambo wa dharura (RSF) yamekuwa yakiukumba mji huo wa pili kwa ukubwa nchini humo, ambao pia ni kituo cha kikamkati kwa jimbo la Darfur.
Makabiliano hayo ya hivi karibuni kabisa yalichukuwa siku tatu mfululizo, huku kila upande ukirusha makombora yake ndani ya makaazi ya raia, kwa mujibu wa mashahidi waliozungumza na shirika la habari la Reuters, ambao wameongeza kuwa mapigano hayo yameharibu mifumo ya umeme, maji na simu.
Soma zaidi: Vita Sudan havionyeshi dalili ya kuisha miezi minne baadae
Amnesty Inernational: Pande zinazozozana Sudan zatenda uhalifu wa kivita
Siku ya Jumamosi (Agosti 12), watu wanane waliuawa, kwa mujibu wa Chama cha Wanasheria wa Darfur, ambacho kinafuatilia pia masuala ya haki za binaadamu.
Chama hicho cha wanasheria kilisema washambuliaji wa makabila ya Kiarabu wakiwa kwenye magari ya RSF walilivamia eneo hilo, wakaliteketeza soko kwa moto na kukivamia kituo cha polisi, wakati wakiwashambulia mahasimu wao ambao pia wana asili ya Kiarabu. Watu 24 walipoteza maisha kwenye uvamizi huo.
"Tunazitaka pande zote kutokujiingiza kwenye mgogoro huu ambao lengo lake ni kuwania madaraka ya nchi." Kilionya chama hicho
Makabila kadhaa ya Kiarabu yametangaza kuwaunga mkono wanamgambo wa RSF kwenye vita hivi na majeshi ya serikali.
Umoja wa Falme za Kiarabu wakanusha kutuma silaha
Hayo yakijiri, Umoja wa Falme za Kiarabu imekanusha ripoti inayodai kwamba kumegundulika silaha kwenye shehena ya misaada kwa wakimbizi wa vita vya Sudan, ikisema kuwa "haiegemei upande wowote" kwenye mgogoro huo.
Mapigano yaliyoanza tarehe 15 Aprili kati ya jeshi na wanamgambo yameshauwa watu 3,900 kwa mujibu wa tathmini inayofuatilia takwimu za migogoro duniani, ACLEDP.
Wafuatiliaji wa mambo wanasema pande zote mbili za vita hivyo - mkuu wa majeshi Abdel-Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo anayeongoza kikosi cha RSF - zinaungwa mkono na mataifa ya kigeni.
Soma zaidi: ICC yaanzisha uchunguzi kwa machafuko ya Sudan
Pande hasimu Sudan zalaumiana kukiuka usitishaji wa mapigano
Nchi jirani, Misri, inashukiwa kumuunga mkono Burhan na Umoja wa Falme za Kiarabu unashukiwa kumuunga mkono Daglo.
Kwenye taarifa aliyoitowa jana Jumapili, mkurugenzi wa mawasiliano kwenye wizara ya mambo ya kigeni ya Umoja wa Falme za Kiarabu alisema kwamba nchi hiyo haijatuma silaha wala risasi kwa pande hasimu za Sudan tangu kuzuka kwa mapigano.
Ripoti iliyochapishwa na gazeti la Wall Street Journal la Marekani siku ya Alkhamis iliwanukuu maafisa wa Uganda wakisema wamegunduwa silaha kwenye ndege ya mizigo ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuelekea kwa wakimbizi wa Sudan nchini Chad mnamo tarehe 2 Juni.
Vyanzo: AFP, Reuters