UAE yakaribisha mpango wa amani wa Marekani kwa Sudan
9 Februari 2026
Umoja wa Falme za Kiarabu umethibitisha hapo jana kuukaribisha mpango wa amani unaoungwa mkono na Marekani kwa ajili ya vita nchini Sudan, ambapo nchi hiyo ya Ghuba imekuwa ikishutumiwa mara kadhaa kuuchochea mzozo huo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa UAE ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba nchi hiyo imeukaribisha mpango kamili wa Amani kwa Sudan uliotangazwa na mshauri mkuu wa Marekani wa Masuala yanayohusu nchi za Kiarabu na Afrika Massad Boulos.
Tangu Aprili 2023, vita kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo wa RSF vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, kuwageuza mamilioni kuwa wakimbizi na kuidumbukiza nchi hiyo kwenye mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.
Hata hivyo, licha ya juhudi mbalimbali za kuvimaliza vita nchini Sudan bado imeshuhudiwa mara kadhaa jitihada hizo zikishindwa kuzaa matunda.