1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UAE yatangaza kujiondoa Muungano wa OPEC

Grace Kabogo Associated Press
29 Aprili 2026

Umoja wa Falme za Kiarabu unajiondoa katika shirika la OPEC ili kuongeza uzalishaji wa mafuta kwa masharti yake, hatua inayomnyima Saudi Arabia mshirika muhimu na kuongeza sintofahamu kuhusu mustakabali wa kundi hilo.

Picha ya mfano ya OPEC | Umoja wa Falme za Kiarabu, Fujairah 2016 | Mwanaume katika kituo cha mafuta wakati wa uzinduzi wa gati
UAE, wakati huo ikiwa sehemu ya Trucial States, ilijiunga na OPEC mwaka 1967Picha: Karim Sahib/AFP

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imetangaza kuwa itajiondoa katika Muungano wa Mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi, OPEC kuanzia Mei 1, 2026, hatua inayotarajiwa kuathiri kwa kiasi kikubwa soko la mafuta duniani.

Tangazo hilo linaiondoa moja ya wazalishaji wakubwa wa mafuta katika kundi hilo, ambalo kwa muda mrefu limekuwa na ushawishi mkubwa katika kudhibiti uzalishaji na bei za mafuta.

Akizungumza Jumanne, Waziri wa Nishati na Miundombinu wa UAE, Suhail Al Mazrouei, alisema uamuzi huo unaendana na mageuzi ya sera ya nishati na mwelekeo wa muda mrefu wa kiuchumi wa nchi hiyo.

Alieleza kuwa hatua hiyo pia inalenga kuwezesha UAE kushirikiana kwa urahisi zaidi na wawekezaji na washirika wa kimataifa katika sekta ya mafuta, gesi na kemikali za petroli.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa uamuzi huo hauchochewi na mvutano wowote na Saudi Arabia, ambayo inaongoza OPEC.

Mapokezi ya Putin Umoja wa Falme za Kiarabu

01:22

This browser does not support the video element.

Athari kwa soko la mafuta

UAE imesema imechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya OPEC, lakini sasa inalenga kuipa kipaumbele maslahi yake ya kitaifa katika sekta ya nishati inayobadilika haraka.

Tangazo hilo pia linajumuisha kujiondoa katika muungano mpana wa OPEC+, unaojumuisha mataifa kama Urusi.

Hatua hiyo inatazamwa kama pigo kwa ushawishi wa OPEC na OPEC+, huku wachambuzi wakitarajia kupungua kwa uwezo wa kundi hilo kudhibiti bei za mafuta kimataifa.

Ingawa uamuzi huo hauhusiani moja kwa moja na hali ya Mlango wa Hormuz, unaweza kuathiri bei ya mafuta ikiwa UAE itaongeza uzalishaji wake.

Siku ya Jumanne, bei ya pipa moja la mafuta ghafi ilikuwa juu ya dola 111, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na viwango vya kabla ya vita.

Watu wakipita karibu na sanamu inayoonyesha pipa la mafuta lenye nembo ya OPEC wakati wa mkutano wa COP29 mjini Baku, Azerbaijan, Novemba 19, 2024.Picha: Maxim Shemetov/REUTERS

Nafasi ya UAE katika OPEC

UAE ilijiunga na OPEC mwaka 1967, na imekuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta ndani ya kundi hilo.

Takwimu zinaonyesha kuwa Februari mwaka huu, UAE ilikuwa ya tatu kwa uzalishaji miongoni mwa wanachama wa OPEC, nyuma ya Saudi Arabia na Iraq.

Kwa ujumla, nchi wanachama wa OPEC huchangia takribani asilimia 36ya uzalishaji wa mafuta duniani na kudhibiti karibu asilimia 80 ya akiba ya mafuta iliyothibitishwa.

Kwa sasa, uamuzi wa UAE unafungua ukurasa mpya katika siasa za nishati duniani, huku athari zake zikitarajiwa kujitokeza katika miezi ijayo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW