1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uagizaji gesi ya Urusi nchini Ufaransa waongezeka maradufu

8 Agosti 2024

Usafirishaji wa gesi asilia ya kimiminika kutoka Urusi kwenda Ufaransa umeongezeka zaidi ya maradufu katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.

Meli ya kusafirisha gesi
Meli ya kusafirisha gesi.Picha: Natalia Kolesnikova/AFP/Getty Images

Takwimu hizo ni kulingana na tathmini mpya ya data za biashara, katika wakati ambapo Ulaya imejaribu kujiondoa kwenye manunuzi ya nishati yanayofadhili vita vya Urusi nchini Ukraine. Ulaya imezuwia uagizaji wa mafuta kutoka Urusi, lakini gesi asili bado inaruhusiwa. 

Serikali za Ulaya zimesema marufuku kamili dhidi ya uagizaji wa gesi ya Urusi inaweza kupelekea gharama za nishati na upashaji joto majumbani kupanda sana, na watumiaji wa viwandani pia wanaweza kuteseka pia.

Uchambuzi huo ulianza kutolewa na taasisi ya uchumi wa nishati na uchambuzi wa kifedha, IEEFA, ambayo ni shirika lisilo la faida lenye makao yake nchini Marekani, iliyo na lengo la kuharakisha mabadiliko ya dunia kuelekea nishati endelevu.

IEEFA ilitathmini data kutoka shirika linalofuatilia safari za meli la Kpler, pamoja na ICIS, ambayo ni taasisi inayotoa data za bidhaa, ambazo kila mmoja ilitoa uchambuzi wake.

IEEFA ilisema kampuni za Ufaransa ziliagiza takribani mita za ujazo bilioni 4.4 za gesi ya LNG kutoka Urusi katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ikilinganishwa na mita za ujazo zaidi ya bilioni mbili katika kipindi sawa mwaka mmoja uliyopita.

Mauzo ya gesi ya Urusi barani Ulaya yamepanda kwa asilimia 7 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.Picha: Vincent Voegtlin/dpa/MAXPPP/dpa/MAXPPP/picture alliance

Na wakati kampuni za Ufaransa ndiyo zinaagiza kiasi kikubwa zaidi cha gesi ya Urusi, uchambuzi mmoja uligundua kuwa mataifa ya Ulaya kwa ujumla yaliagiza asilimia 7 zaidi ya gesi hiyo iliyopoozwa na kuwekwa katika mfumo wa kimiminika kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wake baharini, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka uliyopita.

Waagizaji wengine wakubwa zaidi, Uhispania na Ubelgiji, zilishuhudia ongezeko la asilimia moja na ushukujaji wa asilimia 16 katika uagizaji mtawalia, ilisema IEEFA.

Oleh Savytskyi, mwasisi wa shirika lisilo la faida la Razom We Stand, ambalo linafanya kampeni ya vikwazo zaidi dhidi ya nishati ya visukukuu ya Urusi, alisema lengo la Umoja wa Ulaya la kuondokana na mafuta ya visukukuu ya Urusi kufikia mwaka 2027 lilikuwa linakwenda mrama.

Alisema mataifa yanayonunua LNG kutoka Urusi yanahujumu mabadiliko ya nishati na kuchangia mabilioni kwa juhudi za kivita za Urusi.

Kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa Total Energies ambayo imechangia sehemu kubwa zaidi ya uagizaji kwenye orodha ya mizigo kati ya Januari na Juni ambayo shirika la habari la Associated Press liliona nakala yake, ilisema ilikuwa inafungwa na mikataba iliyosaini kabla ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Hujuma za waasi wa Houthi huko Mashariki ya Kati zatajwa kuwa sababu 

Na wizara ya fedha na uchumi ya Ufaransa ilisema mashambulizi ya waasi wa Kihouthi dhidi ya meli za mizigo zinazopitia Mfereji wa Suezi yamelaazimu kuangaliwa upya uagizaji wa LNG kwa sababu gesi kutoka Mashariki ya Kati haiwezi tena kufikishwa Ulaya kwa urahisi, wakati njia ya Urusi kutokea ncha ya Arctic haijaathiriwa.

Wizara hiyo imebainisha kuwa Ufaransa ni mmoja ya malango makuu ya kuingiza LNG. Ufaransa na Uhispania, kila mmoja ikiwa na vituo saba, ndiyo zenye tamino nyingi zaidi za LNG barani Ulaya.

Waasi wa Houthi wa Yemen wamekuwa wakiilenga misafara ya meli za mizigo kwenye ujia wa maji wa Bahari ya Shamu. Picha: Mohammed Mohammed/Xinhua/picture alliance

Na wakati sawa ambapo Ufaransa ilikuwa inaagiza gesi zaidi ya LNG kutoka Urusi, ilikuwa inaagiza kidogo zaidi kutoka kwa wagavi wengine zikiwemo Marekani, Angola, Cameroon, Misri na Nigeria, mataifa ambayo usafirishaji wake wa LNG haujaathiriwa na mashambulizi ya Bahari ya Shamu.

TotalEnergies ilisema inao wajibu wa kisheria kuheshimu mikataba yake na itafanya hivyo, maadamu serikali za Ulaya zinaichukulia gesi ya Urusi kuwa muhimu kwa usalama wa ugavi wa Umoja wa Ulaya.

Ilisema itasitisha tu uagizaji endapo vikwazo vipya vitawekwa. Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Adalbert Jahnz, alisema uagizaji wa gesi ya Urusi ulishuka pakubwa kati kati ya mwaka 2021 na 2023.

Lakini Savytskyi kutoka Rozam We Stand, ameutolea wito Umoja wa Ulaya kutekeleza kikamilifu marufuku dhidi ya bidhaa hiyo, akisema TotalEnergies haipaswi kuruhisiwa kuendeleza utegemezi wa Ulaya kwa gesi ya Urusi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW