1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika Kusini

Uamuzi wa Afrika Kusini kuipeleka Israel ICC- waibua mjadala

20 Novemba 2023

Uamuzi wa Afrika Kusini wa kuipeleka Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma za uhalifu wa kivita uliofanywa na Israel huko Gaza umeibua mijadala mikali ndani na nje ya nchi.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Sergei Bobylev/imago images/ITAR-TASS

Hatua ya Afrika Kusini kufungua shauri dhidi ya Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC)  imezusha maoni mseto.

Rais Cyril Ramaphosa aliwaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake nchini Qatar siku ya Jumatano kwamba Afrika Kusini imechukua hatua hiyo kwa sababu inaamini kuwa uhalifu wa kivita unafanyika huko Gaza.

Rais Cyril Ramaphosa amesema uhalifu wa kivita anaodai, umekuwa ukifanyika kwa muda mahsusi huko Gaza akitoa mfano wa matukio katika hospitali kubwa ya Gaza ya Al-Shifa.

Israel imekuwa ikisema kuwa kundi la Hamas limekuwa likitumia handaki ya hospitali hiyo kwa operesheni zake, madai yanayokanushwa vikali na kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina.

Soma pia:Miito ya usitishwaji mapigano Gaza yatolewa

Walakini, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) Daniel Hagari amesema siku ya Jumatano kuwa wanajeshi wake waligundua silaha, zana za kivita na vifaa vya kiteknolojia na kijasusi wakati walipofanya operesheni katika hospitali hiyo. Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas ilikanusha taarifa kwamba kulikuwa na silaha katika hospitali hiyo.

Israel imekuwa ikishambulia kwa mabomu maeneo ya Ukanda wa Gaza kwa wiki kadhaa ili kujibu shambulio la kigaidi la Hamas mnamo Oktoba 7, ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine 240 walichukuliwa mateka, kulingana na takwimu za Israel. Hadi sasa zaidi ya watu 13,000 wameuawa huko Gaza, na hii ikiwa ni kulingana na mamlaka inayoongozwa na Hamas.

Ni upi msimamo wa Vyama vya siasa Afrika Kusini?

Chama cha upinzani cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF) kilitoa hoja bungeni siku ya alhamisi ya kutaka ubalozi wa Israel nchini Afrika Kusini ufungwe na uhusiano wa kidiplomasia kusitishwa.

Kiongozi wa chama hicho cha EFF, Julius MalemaPicha: Guillem Sartorio/AFP

Kiongozi wa chama hicho cha EFF, Julius Malema amesema: " kutokana na maadili yetu ya kikatiba ni lazima tusitishe uhusiano huu hadi haki za binadamu za Wapalestina ziheshimiwe, kukuzwa na kulindwa. Ni lazima Israel ifuate sheria za kimataifa, na kabla ya hilo, uhusiano wowote na nchi hiyo lazima uchukuliwe kama kosa kwa katiba yetu."

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress (ANC) kiliidhinisha hoja hiyo ambayo inatarajiwa kupigiwa kura bungeni wiki ijayo.

Msemaji wa ANC, Mahlengi Bhengu, ameeleza katika taarifa kuwa "kutokana na ukatili wa sasa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ANC itakubaliana na hoja hiyo inayoitaka serikali kuufunga ubalozi wa Israel nchini Afrika Kusini na kusitisha mahusiano yote ya kidiplomasia na Tel aviv hadi pale Israel itakapokubali kusitisha mapigano".

Soma pia:Marekani kujadiliana na ICC juu ya uhalifu dhidi ya Putin

Hata hivyo, Corne Mulder kutoka chama cha wazalendo wa kizungu cha Freedom Front Plus (FF+) ameonya dhidi ya hatua hiyo na kusema ukweli wa mambo ni kwamba ukimfukuza balozi wa Israelna kukata uhusiano wote wa kidiplomasia, Afrika Kusini haitakuwa na uwezo wowote wa kuchukua nafasi ya usuluhishi au kuwa na jukumu la kusaidia kumaliza mzozo huo.

Nayo mashirika yanayoiunga mkono Israel yameikashifu serikali ya Afrika Kusini.

Benji Shulman, Mkurugenzi wa Sera za Umma katika Shirikisho la Wazayuni wa Afrika Kusini, ameitaka serikali ya Afrika Kusini kuacha kuingilia haki ya Israel ya kujilinda na badala yake wasaidie kuwezesha kuachiliwa kwa mateka waliotekwa na Hamas.

Nafasi ya Afrika Kusini ni ipi kwa ICC?

Lakini mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Afrika Kusini Kwandile Kondlo anaunga mkono msimamo wa ANC na kusema ikiwa ICC haiwezi kusimama na kuchukua hatua, basi hawana sababu ya kuiamini taasisi hiyo.

Baadhi ya waangalizi wameishutumu Afrika Kusini kwa undumilakuwili kuhusu suala zima la Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.

Wakati ICC ilipotoa ombi kwa Afrika Kusini kutekeleza agizo la kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin iwapo atahudhuria mkutano wa kilele wa BRICS uliofanyika Johannesburg mwezi Agosti, kulikuwa na kauli zinazokinzana kutoka kwa serikali na chama tawala cha ANC - huku wengine wakitaka nchi hiyo kujiondoa kwenye Mahakama hiyo.

Soma pia:Afrika Kusini yapata ukakasi kumkamata Putin

Mabishano kama hayo yaliibuka pia mwaka 2015 wakati Afrika Kusini iliposhindwa kumkamata Rais wa zamani wa Sudan Omar Al Bashir ambaye alikuwa anakabiliwa na waranti wa kukamatwa na ICC, alipohudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Johannesburg.

Amnesty International yataka wanajeshi Myanmar wafikishwe ICC

01:22

This browser does not support the video element.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW