Uamuzi wa kuzaa au la huwahusu watu wawili tu
17 Februari 2009Tukianza na gazeti la RHEIN ZEITUNG na mada ya hifadhi ya data za binafsi inayozusha mabishano nchini Ujerumani,baada ya maelfu ya wafanyakazi kuchunguzwa kwa siri gazeti hilo linaandika:
Mpango wa kuziokoa benki ulioidhinishwa haraka haraka,umedhihirisha kuwa serikali inaweza kupitisha sheria ngumu katika kipindi cha juma moja. Kwanini basi sheria kuhusu hifadhi ya data za wafanyakazi haikuweza kupitishwa katika muda wa miezi michache? Tangu mwaka 2000 Umoja wa Ulaya ulipendekeza sheria kama hiyo katika mwongozo wake wa kuhifadhi data.
Gazeti la FLENSBURGER TAGEBLATT linasema:
Kama suala la hifadhi ya data za waajiriwa lingepewa umuhimu na waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schäuble,basi angechukua hatua za haraka kama alivyofanya kuhusu sheria ya kupambana na ugaidi, uhalifu ulioandaliwa au wapinzani wa katiba.Na mara kwa mara uhuru hukandamizwa kwa sehemu fulani.Lakini mashirika makubwa kama vile Deutsche Bahn,au Telekom yakipeleleza wafanyakazi wake bila ya kuwepo shaka maalum,Schäuble ana wakati wote duniani.
Tukigeukia mada nyingine gazeti la AACHENER ZEITUNG linasema,waziri wa masuala ya familia Ursula von der Leyen ajiulize ikiwa muongezeko mdogo wa idadi ya watoto waliozaliwa unaweza kutazamwa kama ni ufanisi wa kisiasa. na kuongezea:
Watoto zaidi ni neema kwa nchi.Lakini uamuzi wa kuzaa au kutozaa ni uamuzi unaowahusu watu wawili tu bila ya kuwepo ushawishi wa kisiasa. Kwani yeyote atakaeanzisha familia eti kwa sababu ya misaada inayotolewa na serikali,basi anaanzisha familia chini ya msingi dhaifu. Kilicho muhimu ni kuhakikisha kuwa kila mtoto anaezaliwa atapewa nafasi sawa maishani na atakuwa bila ya dhiki au hofu na atatazamwa kwa mapenzi. Hayo ndio yaliyo muhimu-kwani familia iliyo imara huigharimu serikali fedha kidogo kwa sababu familia kama hiyo huleta utulivu,uaminifu na usalama - hayo yanahitajiwa na binadamu ili kuweza kuwa na ufanisi maishani.
Tukiendelea na uhariri wa magazeti ya Ujerumani ndio tunageukia mada inayohusika na nyambizi mbili zilizoepukana na ajali chupuchupu. Gazeti la SCHWAZWÄLDER BOTE linasema hivi:
Bahari ya Atlantik ni kubwa kweli,lakini nyambizi mbili ndogo hazikuweza kupishana kwani huko chini Vanguard na Le Triomphant zimegongana. Wapi hasa imebakia siri.Umma wala usitazamie kupata habari zenye ukweli fulani,hata ikiwa tukio hilo ni aibu kwa serikali nchini Uingereza na Ufaransa.
Gazeti la NEUE OSNABRÜCKER likiiendelea na mada hiyo linasema:
Ni mkasa kuwa nyambizi mbili zenye makombora ya nyuklia zimegongana kama magari mawili kwenye uwanja wa kuegezea magari.Mbali ni hilo bado hakuna hakika kama serikali mjini London na Paris zimeeleza ukweli kamili.
Kwani hadi hivi sasa,habari zinatolewa kidogo kidogo tu.Na hiyo inazidi kusababisha mashaka.