Urusi yasema uamuzi huo utaleta madhara mabaya Syria
26 Machi 2019Urusi ilisema kwamba uamuzi wa Rais Trump bila shaka utaleta madhara mabaya hasa katika mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Syria.
Katika taarifa iliyopeperushwa na shirika la habari la Urusi, rais wa nchi hiyo Vladamir Putin kupitai msemaji wa Ikulu yake Dmitry Peskov alisema Marekani imekiuka sheria za kimataifa na uamuzi huo utaleta madhara mabaya katika mchakato wa amani katika kanda ya Mashariki ya kati na kwa hali ya pekee katika katika mzozo wa Syria.
"Maamuzi ya hivyo bila shaka yatakuwa na matokeo mabaya kwa raia katika mataifa ya Mashariki ya Kati na mazingira yote ya kisiasa katika taifa la Syria. hili halina shaka kabisa kwa mtu yoyote. La muhimu zaidi hii ni hatua nyengine Marekani inachukua waziwazi katika kukiuka sheria za kimataifa. Tunasikitika sana," alisema Peskov.
Kwa upande mwengine rais wa Lebanon Michael Auon aliutaja uamuzi huo kuwa siku ya giza ulimwenguni.
Rais Putin na mwenzake wa Lebanon Auon walitarajiwa kuwa na kikao mjini Moscow kulijadili swala hilo.
Kulingana na shirika la habari la Syria, SANA, maelfu ya watu waliandamana katika mji wa Damascus, Daraa, Sweida na mikoa mengine iliyoko chini ya serikali ya Syria, waume kwa wake walibeba bendera za Syria na mabango yaliyoandikwa ujumbe unaosema Golan ni Syria.
Katika sherehe ndani ya Ikulu ya Marekani siku ya Jumatatu rais wa Marekani Donald Trump alitia sahihi ilani ya kulitambua eneo la Golan kuwa chini ya Israel. Katika sherehe hiyo alikuwepo waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyau.
Israel iliikamata milima ya Golan katika vita vya Mashariki ya Kati mwaka 1967 na mwaka 1981ikaitangaza kuwa eneo lake hatua ambayo haikutambuliwa na jumuiya ya kimatifa.
Marekani ndio taifa la kwanza kutambua Golan kuwa himaya ya Israel.
Mataifa ya Ghuba ya Arabuni ikiwemo Saudi Arabia, Umoja wa Miliki za Kiarabu, Bahrain, Kuwait na Qatar pia zimeupinga uamuzi huo wa Marekani na kuutaja kuwa kizingiti katika mchakato wa kutafuta amani Mashariki ya kati.
Rais wa Iran amesema haiingii akilini kwamba mtu kutoka Marekani anatoa ardhi ya taifa lisilo lake na kuipa ardhi hiyo nchi nyingine.
(RTRE/DPAE/APE)